Yaliyojiri: Wetangula aagiza polisi kueleza aliko Oguda
SPIKA wa Bunge la Kitaifa Moses Wetangula amemuagiza Kiongozi wa Wengi Kimani Ichung’wa kuwasiliana kwa dharura na Inspekta Jenerali Mkuu wa Polisi (IG) Japhet Koome ili kufahamu aliko mchambuzi wa siasa Gabriel Oguda.
Bw Wetang’ula ametoa agizo hilo kufuatia ufichuzi wa Kiongozi wa Wachache, Bw Opiyo Wandayi kuhusiana na madai ya kutekwa nyara kwa Gabriel Oguda, mwanaharakati mashuhuri wa mitandao ya kijamii na mchanganuzi wa sera ambaye anafanya kazi katika ofisi yake.
“Ninaelekeza Kiongozi wa Wengi kuwasiliana na IG na kujua aliko afisa anayefanya kazi katika ofisi ya Kiongozi wa Wachache na kutoa ripoti,” akaelekeza Wetangula.
Agizo la Bw Wetangula linajiri huku kukiwa na shinikizo kubwa kutoka kwa upinzani, kutaka Oguda na wanaharakati wengine waliokamatwa waachiliwe huru.
“Wafanyikazi wako watalindwa chini ya uongozi wangu. Lakini hatutawalinda wale ambao wamevunja sheria,” alisema Spika Wetangula.
Kulingana na Wandayi, Bw Oguda alichukuliwa kutoka nyumbani kwake kwa nguvu asubuhi ya Jumanne, Juni 25, 2024.
Mwanaharakati huyo alifaulu kupiga simu kwa Wandayi saa 2:20 asubuhi, akiripoti kuwa maafisa wa polisi walikuwa wakivamia boma lake.
“Alinipigia simu kwa hofu kubwa, akionyesha kwamba wanaume aliowataja kuwa polisi walikuwa wakiingia kwa nguvu nyumbani kwake. Dakika kumi baadaye, simu yake ilikuwa imezimwa na sikuweza kumpata,” Wandayi alisimulia.