Yaliyomo katika mtihani wa KJSEA hapo Novemba
MNAMO Novemba mwaka huu zaidi ya wanafunzi milioni 1.2 wa Gredi ya 9 watafanya mtihani wa kwanza wa Kenya Junior School Education Assessment (KJSEA), chini ya mfumo wa Elimu ya Umilisi (CBE) kuwawezesha kujiunga na Sekondari Pevu Januari 2026.
Mtihani huo utawasaidia wanafunzi hao, wa kwanza chini ya mfumo huo mpya, kuandama mikondo ya masomo watakayochagua katika kiwango hicho cha masomo.
Mikondo hiyo mitatu ni; Sayansi Jamii, Sanaa na Michezo na Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati (STEM).
Hata hivyo, Shule za Kitaifa zitafundisha mikondo hiyo mitatu kwa sababu zina walimu, vifaa na miundomsingi toshelezi.
Afisa Mkuu Mtendaji wa Baraza la Kitaifa la Mitihani (KNEC), Dkt David Njengere alisema mtihani wa KJSEA utatathmini uelewa mkamilifu wa wanafunzi katika masomo waliofunzwa katika shule ya msingi chini ya mfumo wa CBE kuanzia kiwango cha Gredi 6.
“Tayari walifanya mtihani wa Kenya Primary School Education Assessment (KPSEA), utakaochangia asilimia 20 ya alama. Asilimia 20 nyingine zitatokana na mitihani waliofanya shuleni (School Based Assessments-SBA) katika Gredi 7 na Gredi 8. Mtihani wa KJSEA utachangia asilimia 60 za alama zilizosalia,” Dkt Njengere akaeleza kwenye mahojiano ya kipekee na Taifa Leo.
Aliongeza kuwa wanafunzi katika mikondo ya Sanaa na Michezo tayari wamejipa alama kupitia shughuli kama muziki, drama na riadha ambazo zitaongezea alama za mwisho.
“Katika tamasha ya kitaifa ya muziki katika Ikulu Ndogo ya Sagana, tulishuhudia talanta ya ajabu. Kwa mfano, msichana kutoka Migori aliwasilisha miondoko mizuri zaidi jukwaani. Tayari anaelewa mkondo ambao huenda akafuata,” akasema.