Yego amaliza Olimpiki nambari tano jijini Paris
NYOTA Julius Yego almaarufu YouTube Man amekamilisha Michezo ya Olimpiki katika nafasi ya tano kwa mtupo wa mita 87.72 jijini Paris, Ufaransa.
Arshad Nadeem wa Pakistan, bingwa wa 2020 Neeraj Chopra kutoka India na Anderson Peters wa Grenada wamezoa dhahabu, fedha na shaba baada ya kutupa mkuki mita 92.97, 89.45 na 88.45, mtawalia katika fainali hizo za Alhamisi.
Yego anajivunia mataji matano ya Riadha za Afrika, mawili ya Michezo ya Afrika na moja kutoka Michezo ya Jumuiya ya Madola na dunia.
Afisa huyo wa polisi mwenye umri wa miaka 35 alipata medali ya fedha kwenye Olimpiki mwaka 2016 mjini Rio de Janeiro nchini Brazil.
Yego anashikilia rekodi ya Afrika katika urushaji mkuki baada ya kuandikisha mtupo wa mita 92.72 katika Riadha za Dunia mjini Beijing nchini Uchina mwaka 2015.
Alikuwa akishiriki Olimpiki kwa mara ya nne baada ya kukamata nafasi ya 12 mwaka 2012 mjini London nchini Uingereza, kuzoa medali ya fedha mwaka 2016 halafu akamaliza nambari 24 mwaka 2021 nchini Japan.
Aliingia Olimpiki akijivunia medali mbili za kimataifa mwaka huu baada ya kuzoa fedha kwenye Michezo ya Afrika mjini Accra nchini Ghana mwezi Machi kabla ya kunyakua taji wakati wa Riadha za Afrika mjini Douala nchini Cameroon mwezi Juni.