Habari za Kitaifa

Zawadi ya Ruto kwa wafanyakazi wastaafu na walimu Leba Dei

Na VICTOR RABALLA, MERCY SIMIYU May 2nd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

RAIS William Ruto ameagiza malipo yote ya pensheni na marupurupu ya kustaafu katika sekta ya umma na ya kibinafsi yasitozwe ushuru, katika mabadiliko makubwa ya sera yanayolenga kutambua mchango wa wafanyakazi na wazee nchini.

Aidha, alitangaza walimu wanagenzi 20,000 zaidi wataajiriwa mwaka ujao, Sh3 bilioni za kupandisha vyeo walimu, pamoja na mageuzi katika msamaha wa kodi ili kuongeza mapato ya wafanyakazi.

Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi katika Uhuru Gardens, Rais alisema msamaha huu wa kodi katika pensheni ni sehemu ya juhudi za serikali yake kuhakikisha kuwa wafanyakazi wanastaafu kwa heshima na usalama wa kifedha.

“Mageuzi haya ni kutambua huduma na kujitolea kwa wazee wetu na wafanyakazi. Kustaafu kunapaswa kuambatana na heshima, si mateso,” alisema Rais Ruto.

Msamaha huu wa kodi umetajwa katika Mswada wa Fedha wa mwaka 2025 uliopitishwa hivi karibuni, ambao Rais aliutaja kama nguzo kuu ya ajenda ya mageuzi ya kiuchumi nchini.

Mswada huo unalenga kuongeza uzalishaji, kupanua fursa za kiuchumi, na kupunguza mzigo wa kifedha kwa biashara na wafanyakazi.

Katika hatua nyingine muhimu, waajiri sasa watalazimika kuhesabu moja kwa moja msamaha wa kodi ya mapato ya mshahara (PAYE) kila mwezi, badala ya mfumo wa sasa ambapo mfanyakazi huwasilisha maombi kwa Mamlaka ya Mapato Kenya (KRA).

Rais pia alitaja mafanikio ya mageuzi katika utamaduni wa kuweka akiba, akisema kuwa kanuni mpya za NSSF zilizoanza kutekelezwa mwaka 2023 — zinazohitaji waajiri na wafanyakazi kuchangia asilimia 6 kila mmoja — tayari zimekusanya zaidi ya Sh280 bilioni, kiasi karibu sawa na kilichokusanywa kwa miongo sita iliyopita.

“Tunapanga kufikia zaidi ya Sh1 trilioni ifikapo 2027 na kuongeza kiwango cha akiba kwa Pato la Taifa (GDP) hadi asilimia 25,” aliongeza.

Katika utekelezaji wa Ajenda ya Mageuzi ya Kiuchumi Rais alitaja sekta ya kilimo kama nguzo muhimu ya mapato ya maeneo ya mashambani na usalama wa chakula kitaifa.

Alisema kuwa uzalishaji wa mahindi umeongezeka kwa asilimia 40 kutokana na kupunguzwa kwa bei ya mbolea, na bei ya kahawa imepanda kutoka Sh50 hadi hadi Sh150 kwa kilo kufuatia mageuzi ya sekta hiyo.