Habari

Hafla ya kumtawaza Dkt Nyoro awe Gavana wa tatu wa Kiambu yaahirishwa

January 30th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na LAWRENCE ONGARO

MIPANGO ya kumuapisha Dkt James Nyoro awe gavana wa tatu wa Kaunti ya Kiambu yalitibuka kutokana na mpangilio ya kisheria.

Spika wa kaunti ya Kiambu Bw Stephen Ndichu, ameeleza umati uliofurika katika makao makuu ya Kiambu kuwa wameshauriana na Jaji wa Mahakama Kuu Bw John Onyiego na kupata ya kwamba sheria kamili ilistahili kufuatwa kabla ya kumuapisha naibu gavana Bw Nyoro kwa huo wadhifa wa kuiongoza kaunti.

“Kulingana na sheria, kuna mpangilio maalum unaostahili kufuatwa kabla ya kumuapisha naibu gavana kukitokea utata katika afisi ya gavana. Kwa hivyo, tumepata mwelekeo kutoka kwa Mwanasheria Mkuu Bw Paul Kihara ya kwamba ni sharti mpango huo usitishwe hadi wakati makubaliano yatafanywa,” amesema Bw Ndichu.

Amewataka wote waliohudhuria hafla hiyo wavumilie kwa wakati huu huku majadiliano yakiendelea ili kupanga siku rasmi ambapo naibu huyo wa gavana ataapishwa rasmi.

Wakazi wa Kiambu na wadani wa Dkt Nyoro walikuwa wamefika mapema katika makao makuu ya Kiambu tangu saa moja asubuhi huku wakisubiri kwa hamu kutawazwa kama gavana Dkt Nyoro ambapo hadi saa 8 za mchana bado hakuna lolote lilikuwa nimefanyika.

Baadhi ya viongozi waliofika kushuhudia hafla hiyo ni Seneta maalum, Isaac Mwaura, mwakilishi wa wanawake, Bi Gathoni Wa Muchomba, aliyekuwa mbunge wa Dagoretti Bw Dennis Waweru, Mbunge wa Kiambu Mjini Bw Jude Njomo, naibu gavana wa Nyeri Bi Carolyne Wanjiru, Mbunge wa Ruiru, Bw Simon King’ara, na Mbunge wa Gatundu Kaskazini Bi Wanjiku Kibe, pamoja na madiwani kadha.

Kumekuwa na ulinzi mkali katika lango kuu la kuingia katika makao makuu ya Kiambu na waandishi wa habari wamelazimika kuonyesha vitambulisho vyao kabla ya kuruhusiwa kuingia ndani.

Wafuasi wa Dkt Nyoro waliofika kwenye hafla hiyo wameonyesha nyuso za furaha huku wakiimba nyimbo za kuwaliwaza wakingoja Dkt Nyoro kujitokeza.

Baada ya watu kukaa kwa zaidi ya muda wa saa saba bila kupata ujumbe wowote, Dkt Nyoro alifika mahali hapo huku akishangiliwa na vifijo na vigelegele.

Wafuasi wa Dkt James Nyoro. Picha/ Lawrence Ongaro

Dkt Nyoro amewatuliza wafuasi wake na kuwasihi wavumilie kwani siku rasmi itapangwa ili aweze kutawazwa rasmi Gavana wa Kiambu.

“Hata hivyo, tungetaka sheria iwekwe wazi jinsi naibu gavana anastahili kuchukua mamlaka iwapo kumetokea utata kuhusu afisi ya gavana. Lakini tutaendelea kuchapa kazi kama kawaida,” amesema Nyoro.

Amesema afisi yake itaendelea kutoa basari na kuweka mikataba na washikadau tofauti kwa lengo la kuwafanyia wakazi wa Kiambu kazi.

Mnamo Jumatano Seneti iliamua kwamba Bw Ferdinand Waititu hafai kuwa gavana kufuatia tuhuma za ufisadi.

Baada ya uamuzi huo ndipo iliamuliwa naibu wake Dkt Nyoro ashike usukani mara moja kama gavana wa tatu wa Kiambu.

Hata hivyo kulingana na hali ilivyokuwa mahali hapo wakazi wengi waliofika eneo hilo walionyesha matumaini ya kupata kiongozi mwingine baada ya Bw Waititu kung’atuliwa.

Naye Waititu amewasilisha katika mahakama ya Nairobi kesi kupinga kubanduliwa kwake. Jaji wa Mahakama Kuu James Makau ameiratibu kesi hiyo kuwa ni ya dharura na akaagiza nakala za kesi zikabidhiwe upande ulioshtakiwa kufikia Ijumaa mchana  kabla ya kusikizwa kwa kesi Jumatatu wiki ijayo.

Waititu anataka kuapishwa kwa Naibu Gavana kusitishwe, utekelezwaji wa uamuzi wa seneti usitishwe na kwamba naibu wake azuiwe kutekeleza majukumu ya gavana. Pia anataka notisi ya gazeti rasmi la serikali kuhusu kubanduliwa kwake nayo isitishwe.

 

Taarifa zaidi na Maureen Kakah