Haji aagiza aliyemchinja mbwa akala nyama yake aachiliwe
Na ALEX NJERU na CHARLES WASONGA
MKURUGENZI wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji ameamuru kuachiliwa huru kwa mwanamume aliyekamatwa kwa kumchinja mbwa ambapo alipika nyama yake na kuila katika Kaunti ya Tharaka Nithi mnamo Alhamisi.
Katika ujumbe aliotuma kupitia akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa Twitter, Haji pia aliamua Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) George Kinoti kuhakikisha mwanamume huyo anapata chakula cha kutosha.
John Munene alikamatwa nyumbani kwake katika kijiji cha Karimba, kaunti ndogo ya Maara na maafisa wa polisi kwa kumchinja mbwa na kuupika mnofu wake kwa lengo la kuila.
Bw Munene alisema alichukua hatua hiyo kwa kukaa siku tatu bila chakula. Alieleza kuwa aliona aibu kuomba chakula kila mara kutoka kwa majirani zake.
“Nilikuwa nikipika nyama ya mbwa ili nile kwa ugali mdogo ambao nilikuwa nimepika,” akasema
Mwanamume huyo alizuiliwa katika Kituo cha Polisi cha Chogoria kabla ya kuwasilishwa mahakamani mjini Chuka leo Ijumaa.
Sehemu ya 3 (3) ya Sheria inayopinga Ukatili dhidi ya Wanyama inasema kuwa mtu aliyepatikana kumdhulumu mnyama ataadhibiwa kwa kutozwa faini isiyozidi Sh3,000 au kifungo kisichozidi miezi sita gerezani au adhabu zote mbili.
Bw Nicholas Mutembei ambaye ni mkazi wa eneo hilo amewaambia wanahabari kwamba kitendo hicho kiliwashangaza wanakijiji kwani ilikuwa ni mara ya kwanza kushuhudiwa hapo.
Baa la njaa linashuhudiwa maeneo kadhaa nchini kufuatia kiangazi cha kipindi kirefu baada ya msimu wa mvua fupi kuchelewa.