Habari

Hakimu ajiondoa katika kesi akihofia maisha yake

Na DAVID MUCHUI October 31st, 2025 Kusoma ni dakika: 1

HAKIMU Mkuu wa Tigania, James Macharia, amejiondoa kusikiliza kesi inayomkabili mfanyabiashara wa Meru anayeshtakiwa kwa kumwagia maji moto msichana wa miaka 15, akitaja vitisho dhidi ya maisha yake na hasira kubwa za umma kuhusu tukio hilo.

Hakimu huyo, ambaye alitarajiwa kutoa uamuzi wa ombi la dhamana kwa mshtakiwa Morris Gitonga, aliamua kuhamisha kesi hiyo hadi Mahakama ya Meru kwa usalama wake binafsi na wa wahusika wengine.

Gitonga alifikishwa mahakamani Jumanne na kushtakiwa kwa kumjeruhi vibaya msichana huyo nyumbani kwake katika soko la Kianjai, kaunti ndogo ya Tigania. Alikana mashtaka na akaomba kuachiliwa kwa dhamana.

Afisa anayechunguza kesi Ann Chege aliomba mahakama imnyime dhamana mshtakiwa ili “asihatarishe au kuwatisha mashahidi.”

Lakini Ijumaa, Hakimu Macharia alisema mazingira ya mahakama ya Tigania hayakuwa salama kwa kuendelea na kesi hiyo.
“Kuna hasira kubwa za umma kuhusu kesi hii, hasa kupitia mitandao ya kijamii. Mazingira haya ni hatari, si kwangu tu bali pia kwa upande wa mashtaka. Si salama kesi hii kuendelea hapa,” alisema Macharia.

Alifichua kuwa amekuwa akipokea simu za vitisho na kwamba ripoti za kiusalama zimeonya kuna hatari kwa maisha yake.
“Kwa misingi ya uwajibikaji, haki na usalama, naelekeza kesi hii isikilizwe katika Mahakama ya Meru. Faili ya kesi itapelekwa huko kwa mwelekeo zaidi,” akaongeza.

Mahakama iliamuru Gitonga azuiliwe katika Gereza la Meru kwa siku 14 akisubiri kutajwa kwa kesi hiyo Novemba  17 2025.

Kulingana na polisi, msichana huyo wa miaka 15 kutoka kijiji cha Mailu, eneo la Tigania Magharibi, alifungwa kamba na kumwagiwa maji moto mnamo Septemba 28, 2025, jambo lililosababisha majeraha mabaya tumboni, kifuani, mgongoni na miguuni.

Tukio hilo limezua ghadhabu kubwa ya wananchi, huku polisi wakilaumiwa kwa kuchelewa kuchukua hatua.

Wanaharakati wa haki za binadamu na watumiaji wa mitandao ya kijamii wameitisha maandamano katika soko la Kianjai Jumapili, wakitaka haki itendeke kwa manusura huyo.