Habari

'Hakuna hoja ya kumbandua Dkt Ruto'

May 25th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA

BUNGE la kitaifa limeitaja kama feki nakala ya shughuli za bunge inayozungushwa mitandaoni na inayodaiwa kuorodhesha hoja maalum ya kumtimua afisini Naibu Rais William Ruto.

Kwenye taarifa aliyoitoa Jumatatu, karani wa bunge hilo Michael Sialai amepuuzilia hati hiyo akidai inalenga kuwapotosha wabunge na umma kwa ujumla.

Stakabadhi hiyo inadai kuwa miongoni mwa makosa yanayosababisha kuondolewa afisini kwa Dkt Ruto ni ukiukaji wa Katiba na mienendo isiyokubalika.

Mjadala kuhusu hoja hiyo ndio shughuli ya kipekee iliyoorodheshwa mnamo Juni 2, 2020, bunge litakaporejelea vikao baada ya likizo iliyoanza mnamo Mei 6, 2020.

Bw Sialai hata hivyo amesema hakuna mbunge ametoa ilani ya hoja yoyote maalum kwa afisi yake au ile ya Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi.

“Na hakuna orodha ya wabunge au sahihi zao za kuunga mkono hoja kama hiyo katika afisi hizo mbili,” karani huyo akasema.

Mbunge wa Kieni Kanini Kega ndiye ameorodheshwa kama mdhamini wa hoja hiyo iliyosambazwa.

Akijitenga na hoja hiyo, mbunge huyo ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Biashara, amedai wandani wa Dkt Ruto ndio wameanzisha maneno na uvumi wa kusema analengwa kuenguliwa.

“Hii ni njama ya kuchochea umma na kuchora taswira kwamba kuna mpango wa kummaliza Dkt Ruto kisiasa. Ningependa kufafanua kuwa hatuna hoja ya kumng’oa mamlakani Naibu Rais. Hiyo sio ajenda yetu,” Bw Kega akasema.