Hakuna nusu mkate, Duale afafanua
Na CHARLES WASONGA
Kiongozi wa wengi katika Bunge la Kitaifa Aden Duale Jumatano alisema muungano wa upinzani bado utakuwa ukiendelea kutekeleza wajibu wake wa kupiga msasa utendakazi wa serikali ndani na nje ya bunge huku ukishirikiana na serikali kutatua changamoto zinazowakabili Wakenya.
Akichangia hoja kuhusu mwafaka kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga, mbunge huyo wa Garissa Mjini, alibainisha kuwa mwafaka huo haumaanishi kuwa upinzani umejiunga na serikali, au kutabuniwa serikali ya mseto.
“Hakuna serikali ya nusu mkate hapa. Ieleweke kuwa Rais Uhuru Kenyatta na Mheshimiwa Raila Amollo Odinga hawakuungana kwa ajili ya kugawana mamlaka. Chama cha ODM, chake Bw Odinga na vyama vingine tanzu ndani ya NASA bado vitasalia kuwa upande wa upinzani na kuchunguza utendekazi wa serikali ya Jubilee,” akasema Bw Duale.
“Huu mwafaka kati ya viongozi hawa wawili umejengwa katika msingi wa kupalilia amani, umoja na maridhiano kwa lengo kuu cha kuimarisha uchumi wa nchi hii. Wenzetu hata hivyo wataungana nasi kutekeleza ajenda za maendeleo ya Jubilee,” akaongeza mbunge huyo.
Bw Duale aliunga mkono hoja hiyo iliyowasilishwa na kiongozi wa wachache John Mbadi akiwataka wabunge kuunga mkono hatua ya Rais Kenyatta kuzika tofauti zao na kufanya kufanya pamoja kuunganisha nchini.
Kiongozi huyo wa wengi pia alipuuzilia mbali dhana kwamba mwafaka kati ya Rais Kenyatta na Bw Odinga utavuruga mpangilio wa urithi wa uongozi katika chama cha Jubilee.
Kulingana na Bw Duale mpango wa Jubilee kwamba Naibu Rais William Ruto ndiye mrithi wa Rais Uhuru Kenyatta, utasalia vivyo hivyo kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022.
“Ningependa kufafanua kuwa hatua hii haitaathiri kwa vyovyote uamuzi wa Jubilee kwamba William Ruto ndiye atapeperusha bendera yake 2022. Wanaotaka kuungana na Jubilee wanaalikwa lakini sharti wakubali kuchukua nyadhifa zingine za chini kwani ule wa juu tayari una mwenyewe,” Duale akaeleza.
Akiwasilisha hoja rasmi, Bw Mbadi ambaye ni Mbunge wa Suba Kusini alipongeza ushirikiano kati ya Rais Kenyatta na Bw Odinga akisema utaunganisha taifa na kuimarisha ukuaji wa uchumi.
“Ningependa kusema kuwa hatua hii ya kizalendo ilijiri wakati ambapo taifa hili lilikuwa limegawanyika. Sasa mwafaka umepatikana na sote tunafaa kushirikiana kuijenga nchini kwa manufaa ya Wakenya na vizazi vijavyo,” akasema Bw Mbadi ambaye kwa mara ya kwanza alimtambua Kenyatta kama Rais halali.
Hoja hiyo iliungwa mkono kwa kauli moja na wabunge kutoka mirengo yote miwili ambao kwa mara ya kwanza waliwasifu Rais Kenyatta na Bw Odinga bila kuzingatia miegemeo yao ya kisiasa.
Bw Mbadi, ambaye ni mwenyekiti wa ODM pia alisema kuwa mwafaka kati ya Raila na Uhuru haumaanishi kuwa upinzani umejiunga na serikali au utabuni serikali ya muungano.