HAPA KUNA KITU: Je, mkutano wa Uhuru, Raila utamchochea kukataa dili ya Ruto?
MKUTANO wa ghafla kati ya aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga huku pakiwepo shinikizo atie saini mkataba wa kisiasa na Rais William Ruto, umeibua maswali mapya kuhusu mwelekeo atakaofuata kiongozi huyo wa ODM.
Bw Kenyatta na Bw Odinga Jumatatu walikaribishwa na makamu mwenyekiti wa chama cha Jubilee, Bw David Murathe katika hoteli yake iliyoko Watamu, Kilifi.
Mkutano huo ulihudhuriwa na Gavana wa Kilifi, Gideon Mung’aro, ambaye alikuwa na waziri mkuu huyo wa zamani katika mikutano yake inayoendelea ya mashauriano na wafuasi wa ODM katika kaunti hiyo.
Mkutano huo wa siri ambao umeibua hisia za kisiasa ulifanyika wakati ambapo chama cha Rais Ruto cha United Democratic Alliance (UDA) kimeitisha mkutano wa Kamati yake ya Kitaifa ya Uongozi – ambao kwa kawaida unaongozwa na kiongozi wa chama – leo asubuhi.
Mkutano huo unatarajiwa kujadili maelezo ya makubaliano ya kisiasa yanayotarajiwa kati ya UDA na ODM huku afisa mkuu wa Ikulu akiambia Taifa Leo kwamba mkataba huo unaweza kutiwa saini Ijumaa hii.
Bw Murathe alithibitisha mkutano wa Watamu lakini akakanusha majadiliano yoyote kuhusu siasa. Alisema kwamba Bw Odinga alienda kumuona Bw Kenyatta katika hoteli hiyo, akisisitiza kwamba mkutano huo haukupangwa.
“Baba (Raila) alikuwa Kilifi kwa mikutano yake ya ODM. Alifahamishwa kuwa Uhuru alikuwa karibu na akaja. Haikuwa imepangwa kamwe,” akasema Bw Murathe.
“Alikuja na Gavana Mung’aro, lakini yeye (gavana) aliondoka mapema zaidi. Mimi kama mwenyeji, niliwapa chai,” alisema Afisa mwingine wa ODM, ambaye alizungumza kwa sharti asitajwe, alisema kuwa Bw Odinga alikutana kisadfa na Bw Kenyatta, ambaye alidai amekuwa Kilifi kwa wiki moja iliyopita.
“Hakukuwa na mkutano uliopangwa. Walikutana tu hotelini,” afisa huyo alisema.Hata hivyo, wadadisi wa siasa walikuwa wepesi kurejelea nukuu maarufu ya Rais wa zamani wa Amerika Franklin D Roosevelt kwamba katika siasa, hakuna kinachotokea kwa sadfa.’Ikitokea, unaweza kuamini ilipangwa kuwa hivyo,” Roosevelt alinukuliwa akisema.
Tangu wiki jana, Bw Odinga amekuwa akishauriana na marafiki na wafuasi wake kabla ya kuamua mwelekeo wa kisiasa kuhusu iwapo atashirikiana na Rais Ruto au la.
“Nimerudi nyumbani, nitakutana na marafiki zangu, wafuasi wangu, na nitaenda kushauriana kwa upana. Baadaye tutatangaza njia ya kusonga mbele,” akasema Bw Odinga, alipokaribishwa na Rais Ruto katika Ikulu, Mombasa.
Chama cha ODM kimepanga kuandaa kikao kingine cha Kamati Kuu ya Usimamizi wiki hii ili kuamua msimamo kuhusu suala hilo.
Alhamisi iliyopita, kamati ilifanya mkutano wake wa kwanza mjini Kisumu kujadili kuhusu mapendekezo ya ushirikiano na chama cha Dkt Ruto cha UDA.
Inasemekana katika mkutano huo, kamati iliunda kikosi cha kiufundi kinachoongozwa na Prof Adams Oloo.
Pia katika kikosi hicho kina wakili Jackson Awele na mawakili wengine wa ODM.
Kikosi hicho, kulingana na afisa wa ODM ambaye alizungumza kwa sharti asitajwe, kimepewa jukumu la kupitia rasimu ya makubaliano ya ushirikiano.
Kikosi hicho cha kiufundi kinatarajiwa kuripoti kwa Katibu Mkuu wa ODM, Edwin Sifuna, ambaye baadaye atawasilisha ripoti hiyo mbele ya Kamati Kuu ya Usimamizi ya chama ili kuidhinishwa.
Bw Sifuna, hata hivyo, angali anakosoa utawala wa Rais Ruto na amekuwa akisema mara kwa mara kuwa kiongozi huyo atashindwa hata iwapo ataungwa mkono na Bw Odinga.
Rais Ruto na Bw Kenyatta wanaonekana kuwania Bw Odinga kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2027 ambapo waziri mkuu huyo wa zamani huenda akawa na nguvu kwenye kinyang’anyiro cha urais.