Harusi ya mwaka
Na GEORGE MUNENE na WANDERI KAMAU
HATIMAYE Gavana Anne Waiguru wa Kirinyaga, alifanya harusi ya kukata na shoka na wakili Kamotho Waiganjo, sherehe ya Jumamosi ambayo ilihudhuriwa na watu maarufu, akiwemo Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga.
Viongozi hao waliungana na wanasiasa, jamaa na marafiki kushuhudia harusi ya kitamaduni ya Gavana huyo iliyofanyika katika Shule ya Msingi ya Kiamugumo, eneobunge la Gichugu, Kaunti ya Kirinyaga.
Watu wengine maarufu waliohudhuria harusi hiyo ni kiongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka, mawaziri, makatibu wa wizara na wabunge zaidi ya 50.
Baadhi ya maseneta waliofika ni James Orengo (Siaya), Ledama Ole Kina (Narok), Njeru Ndwiga (Embu), wawakilishi wa wanawake Florence Mutua (Busia), Sabina Chege (Murang’a), Fatuma Gedi (Wajir) kati ya wengine.
Gavana Muthomi Njuki wa Tharaka Nithi pia alikuwepo.
Wageni walianza kufika alfajiri na mapema wakijawa na furaha kusherehekea harusi hiyo iliyofanywa kwa kuzingatia desturi ya jamii ya Akikuyu.
Shule hiyo pia ilirembeshwa vilivyo, huku viti vikiwa vimepangwa vizuri jukwaani kuwapokea wageni.
Na ikizingatiwa harusi hiyo ilikuwa ya kitamaduni, kulingana na jamii ya Agikuyu, Bi Waiguru na Bw Waiganjo walikuwa wamevaa mavazi maalum ya rangi ya kahawia.
Wawili hao pia walijifunga mashuka maalumu ya rangi hiyo, kuashiria umuhimu wa hafla hiyo.
Wageni wengi vilevile walivaa mavazi ya rangi hiyo, kulingana na tamaduni za harusi za jamii hiyo.
Vyakula vya kienyeji kama Uji (Ucuru wa Mukio) ‘Mukimo’, Ngwaci (viazi vitamu) na pombe (Muratina) pia vilikuwepo.
Wageni pia walifurahia nyama ya ng’ombe, mbuzi na kuku ambayo pia ilikuwa imechomwa na kupikwa kwa njia ya kitamaduni. Wacheza densi pia waliipamba hafla hiyo kwa kuimba nyimbo za kitamaduni za jami ya Agikuyu kama ‘Mwomboko’ na ‘Muugithi’, ambazo huimbwa katika hafla za harusi.
Upeo wa hafla hiyo ulikuwa wakati nyama maalumu ya kondoo iliyochomwa ilikatwa, maarufu kama ‘ngurario’ kuashiria kuwa wawili hao ni mume na mke. Awamu hiyo ndiyo ya mwisho kuashiria kuwa mchakato wa wawili hao kuunganiswa kuwa mume na mke ulikuwa umekamilika.
Mamia ya wageni waliohudhuria, wengi wao wakiwa wanawake, walishangilia kwa vifijo.
Baadaye, kibarua cha Bw Waiganjo kilikuwa kumtambua Bi Waiguru kama mkewe halisi kutoka kwa wanawake kadhaa ambao huwa wamefichwa nyuso zao.
Furaha ilizidi alipofaulu kumtambua.
Hilo pia huwa hitaji kuu katika tamaduni za jamii hiyo.
Hafla ilipoisha, wageni walioalikwa walipewa nafasi ya kutoa zawadi zao kwa maharusi.
Wawili hao walikutana na kujuana miaka kumi iliyopita katika eneo la Likoni, Mombasa, wakiwa katika shughuli zao za kikazi. Walianza urafiki uliokomaa hadi wakafikia kuoana.
Wakazi mbalimbali waliisifu hafla hiyo, wakisema imechangia sana kuimarishwa kwa miundomsingi kama barabara eneo hilo.