HATIMA YA SONKO: Lusaka awaita maseneta wote
Na CHARLES WASONGA
MASENETA Jumatano wataanza kusikiliza mashtaka dhidi ya Gavana wa Nairobi Mike Sonko ambayo yalisababisha madiwani wa kaunti hiyo kupitisha hoja ya kumwondoa afisini mnamo Desemba 3, 2020.
Spika wa Seneti Kenneth Lusaka amechapisha ilani kuhusu kikao maalum cha kujadili hatima ya Gavana huyo ambaye pia anazongwa na msururu wa kesi za ufisadi kortini.
Alisema kuwa maseneta wote 67 watashiriki katika kikao cha Jumatano na kingine cha Alhamisi, kuamua hatima ya Bw Sonko ambaye madiwani wanataka aondolewe afisini kwa kukiuka katiba, kutumia mamlaka ya afisi yake vibaya na kukiuka sheria kadha zikiwemo zile za utoaji zabuni za umma.
Haya ndio mashtaka makuu yaliyomo katika hoja ya kumtimua Sonko afisini, hoja ambayo ilidhaminiwa na kiongozi wa wachache Michael Ogada.
Hoja hiyo iliungwa mkono na madiwani 88 kati ya 122 hatua ambayo ilipingwa na Sonko pamoja na wandani wake waliodai kuwa jumla ya madiwani 59 hawakuwepo bungeni siku hiyo.
Hata hivyo, ilisemekana kuwa Spika wa Bunge hilo Benson Mutura aliwaruhusu madiwani kushiriki mjadala kuhusu hoja hiyo na hatimaye kupiga kura zao kwa njia ya mtandao.
Baadhi ya waliodaiwa kupiga kura ya kuunga mkono kutimuliwa kwa Sonko ni madiwani wandani wake ambao aliwasafirisha hadi nyumbani kwake katika Kaunti ya Kwale ili kuzuia uwezekano wa kupatikana kwa thuluthi mbili ya madiwani kushiriki upigaji kura inavyohitajika kisheria.
Baadhi ya madiwani hao, wandani wa Gavana Sonko, hata hivyo walidai kuwa Spika Mutura aliwaruhusu wafanyakazi wa bunge hilo kupiga kura kwa niaba yao.
Hatima ya gavana huyo itaamuliwa na kikao cha maseneta wote baada ya Kiongozi wa Wengi Samuel Poghisio wiki jana kudinda, dakika za mwisho, kuwasilisha rasmi hoja iliyopendekeza kubuniwa kwa kamati maalum ya maseneta 11 kuchambua uhalali wa mashtaka hayo.