Habari

Hatima ya Waititu kuamuliwa wiki ijayo – Lusaka

January 23rd, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA

HATIMA ya Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu Baba Yao aliyekataliwa na madiwani wa kaunti hiyo sasa itaamuliwa na maseneta katika vikao vitakavyofanyika Jumanne na Jumatano juma lijalo, Spika wa Seneti Kenneth Lusaka.

Hii ni baada ya madiwani wa bunge la kaunti hiyo kupitisha hoja ya kumwondoa mamlakani Gavana Waititu Desemba 19, 2019, hatua ambayo, kikatiba, inafaa kuidhinishwa au kukatiliwa na Seneti.

Kwenye mahojiano na ‘Taifa Leo’ Bw Lusaka amesema Alhamisi kwamba ameitisha vikao maalum siku hizo mbili ambapo madiwani wa Bunge la Kaunti ya Kiambu na Gavana Waititu wamealikwa wahudhurie.

“Nitachapisha ilani kwenye gazeti rasmi la serikali leo (Alhamisi) kuitisha vikao maalum vya seneti Januari 28 na 29 kwa ajili ya kujadili na kuamua kuhusu hoja ya kumwondoa Gavana Ferdinand Waititu,” amesema Lusaka.

Akaongeza: “Na madiwani wa Bunge la Kiambu pamoja na Bw Waititu wameagizwa kuhudhuria vikao hivyo, uhalali wa mashtaka hayo utakapojadiliwa na maseneta wote 67.”

Katika kikao cha Jumanne wiki hii, maseneta walitupilia mbali hoja ya kuundwa kwa kamati maalum ya kuchambua mashtaka dhidi ya Waititu.

Maseneta, wengine wao kutoka mrengo wa Jubilee, walikataa orodha ya wanachama wa kamati hiyo iliyowasilishwa na kiongozi wa wengi Kipchumba Murkomen, wakisema “ilijaa maseneta wa mrengo wa ‘Tangatanga’.

Na kura ilipigwa kuamua suala hilo, maseneta wa mrengo wa ‘Kieleweke’ waliungana na wenzao wa upinzani kuunga mkono pendekezo kwamba suala hilo lishughulikiwe katika kikao cha bunge lote la seneti.

Kulingana na orodha iliyosomwa na Bw Murkomen, upande wa Jubilee uliwakilishwa na kiranja wa wengi Susan Kihika (Nakuru), Sylvia Kasanga (Seneta maalum), Hargura Godana (Marsabit), Aaron Cheruiyot (Kericho), Anuar Oloitipitip (Lamu) na Mithika Linturi (Meru).

Na katika mrengo wa upinzani ulikuwa uwakilishwe na; Cleophas Malala (Kakamega), Mohamed Faki (Mombasa), Oman Farhada (Seneta Maalum), Fred Outa (Kisumu) na Okong’o Omogeni (Nyamira).