Habari

Hekaheka Kisii Matiang’i akianza misafara ya kukutana na wafuasi

Na WYCLIFFE NYABERI May 2nd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

ALIYEKUWA Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i anatarajiwa kuzuru ngome yake ya Gusii hii leo Ijumaa kwa mara ya kwanza tangu aliporejea nchini kutoka Amerika.

Dkt Matiang’i anasemekana kumezea mate kiti cha urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

Ziara yake ya nyumbani imefasiriwa na wengi kuwa mwanzo wa kampeni zake, kujiweka tayari kwa kinyang’anyiro kikali dhidi ya Rais William Ruto.

Kulingana na ratiba iliyotolewa na wandani wa waziri huyo aliyehudumu chini ya Rais mstaafu Uhuru Kenyatta, Dkt Matiang’i atahutubia wafuasi wake katika mikutano ya kando ya barabara.

Msafara wa waziri huyo wa zamani utaanzia mji wa Kijauri, ambako ndiko nyumbani kwa Dkt Matiang’i.

Msafara huo utaelekea katika miji ya Keroka, Keumbu na hatimaye kutua Kisii ambapo atahutubia umati mkubwa wa watu.

Katika ziara hiyo, Dkt Matiang’i anatarajiwa kusindikizwa na wabunge kutoka eneo la Kisii wanaounga azma yake ya ikulu.

Tayari, wakazi wengi wa Gusii wamechangamkia ziara ya kiongozi huyo ambaye anapigiwa upatu kurithi viatu vya aliyekuwa kigogo wa siasa za Gusii, marehemu Simeon Nyachae.

Tangu kifo cha Nyachae mwaka 2022, jamii ya Abagusii haijawahi kuwa na kiongozi shupavu wa kutetea maslahi yao kama alivyokuwa akifanya Nyachae.

“Tuna furaha kuwa mwana wetu, Dkt Fred Matiang’i hatimaye anarejea nyumbani. Tunamkaribisha kwa moyo mkunjufu na tunatarajia atatutangazia rasmi kuwa atakuwa katika kinyang’anyiro cha kuwania urais katika uchaguzi ujao,” Elijah Okindo, mkazi wa Bobaracho katika eneobunge la Nyaribari Chache alihoji.

Bw Okindo alitoa onyo kwa wanasiasa wengine wa Gusii wanaompinga Dkt Matiang’i, akidokeza kuwa wapigakura watawaadhibu ikiwa wataenda kinyume na uamuzi wa kisiasa wa 2027 utakaotolewa na jamii.

Bw Okindo alieleza kuwa, wanasiasa waliokuwa wakimpinga marehemu Nyachae wakati huo, hawakuchaguliwa na wenyeji.

“Nyachae alipowania urais mwaka 2002, alishinda viti vyote vya ubunge eneo la Gusii kupitia chama chake cha Ford People. Wakati mwingine kama ule wa Nyachae umefika,” Bw Okindo aliongeza.

Alipokuwa Ughaibuni, Dkt Matiang’i alikuwa akipigiwa debe kuwa ndiye chaguo sahihi kumkabili rais Ruto katika uchaguzi ujao na vyama vya Jubilee na United Progressive Alliance (UPA).

Vyama hivyo vyote viwili vimekwishatangaza kuwa Dkt Matiang’i atakuwa debeni kuwania urais.

Mnamo Jumanne wiki hii, Dkt Matiang’i aliungana na viongozi wengine wa upinzani kupanga mikakati kuhusu umoja wao.

Mkutano huo uliwakutanisha waziri huyo wa zamani, kiongozi wa chama cha People’s Liberation Party (PLP) Martha Karua, kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, kiongozi wa Democratic Action Party of Kenya (DAP-K) Eugene Wamalwa na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua.

Pia katika mkutano huo, alikuwepo mwanasiasa Dkt Mukhisa Kituyi na mawaziri wawili waliofutwa katika serikali ya rais Ruto Mithika Linturi na Justin Muturi.