Hisia mseto kuhusu BBI
Na CHARLES WASONGA
VIONGOZI wa kisiasa Alhamisi waliibua hisia mseto kuhusu ripoti ya BBI baada ya kuzinduliwa kwa shughuli ya ukusanyaji wa sahihi kuunga mkono marekebisho ya Katiba.
Huku baadhi yao wakiunga mkono mswada huo wa marekebisho ya Katiba wengine walishikilia kuwa taifa haliko tayari kwa kampeni za kisiasa haswa wakati huu wa janga la corona
Kiongozi wa Chama cha Amani National Congresss (ANC) Musalia Mudavadi Alhamisi alisema kuwa mengi ya masuala tata ambayo aliibua yameshughulikiwa.
“Nilihudhuria hafla ya uzinduzi rasmi wa ukusanyaji wa sahihi katika ukumbi wa KICC ambako mswada wa BBI ulizinduliwa. Tathmini yangu ya haraka ilionyesha kuwa masuala ambayo mimi na Wakenya wengine tuliibua yameshughulikiwa kwa kiwango kikubwa,” akawaambia wanahabari katika kituo cha Musalia Mudavadi Centre kilichoko Riverside, Nairobi.
Seneta wa Makueni Mutula Kilonzo Junior pia aliunga mkono kauli ya Bw Mudavadi akisema mengi ya mapendekezo yaliyoibua utata na pingamizi yaliondolewa kwenye ripoti ya mswada wa BBI wa awali.
“Mswada wa Marekebisho ya Katiba wa 2020 umeboreshwa kuliko rasimu ya zamani. Mengi ya masuala tata kama vile kuongezwa kwa idadi ya maeneobunge, mamlaka ya Seneti, Uteuzi wa Afisi ya Afisa wa kupokea malalamishi kuhusu majaji, suala la ugavi wa fedha kati ya serikali kuu na zile za kaunti na kuhamishwa kwa majukumu ya Kaunti ya Nairobi hadi Serikali Kuu sasa yamewekwa bayana,” akasema Bw Kilonzo Junior ambaye pia ni kiranja wa wachache katika seneti.
Mbunge Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti ya Homa Bay Gladys Wanga alisema rasimu ya mwisho ya ripoti ya BBI imeshughulikia suala ya uwakilishi wa jinsia bungeni.
“Tangu taifa hili lijinyakulie uhuru, tumepambana na suala hili la usawa wa jinsia bila mafanikio. Ni furaha yetu kama wanawake kwamba BBI sasa imelishughulikia kwa ukamilifu. Huu ni ushindi kwa wanawake wa Kenya,” akasema.
Lakini Seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen, Aaron Cheruiyot (Kericho) aliyekuwa Mbunge wa Mukurweini Kabando wa Kabando na Wakili mashuhuri Ahmednasir Abdullahi walipinga ripoti hiyo wakisema haijashughulikia matakwa ya Wakenya.
“Chini ya BBI bunge litakuwa na angalau wabunge 520 ndani ya miaka 15 ijayo huku bunge la Kitaifa likiwa na kati ya wajumbe 420 na 430,” akasema Murkomen ambaye ni mwandani wa karibu wa Naibu Rais William Ruto.