Hiyo ni yako! Viongozi wa Kanu Baringo wajitenga na muafaka wa Ruto, Moi
BAADHI ya viongozi wa Kanu katika Kaunti ya Baringo wameonyesha kutoridhishwa na makubaliano ya kisiasa kati ya United Democratic Alliance (UDA) na mwenyekiti wao, wakidai kuwa Gideon Moi alianzisha muungano huo peke yake bila kushauriana na uongozi wa chama.
Viongozi hao walieleza kutofurahishwa na mabadiliko hayo ya ghafla, wakisema kuwa Baraza Kuu la Kitaifa (NEC) halikushirikishwa.
Kikosi kinachoongozwa na Mwenyekiti wa Kanu Baringo Kaskazini, Elijah Kandie, kilieleza kuwa waliitwa kuhudhuria kikao Kabarak Oktoba 10, 2025, kutangaziwa “habari mpya” kwamba Seneta wa zamani wa Baringo alikubali muungano na UDA.
“Hatukupewa muda wa kuhoji muungano huu. Ni jambo la kutamausha kuona wa chama chetu kikosa mwelekeo. Wanachama wa KANU waliokuwepo Kabarak na Rais William Ruto wanajuta kwa kitendo cha mwenyekiti wetu kuunda muungano na UDA,” alisema Kandie.
Walisema pia kuwa kujiondoa kwa Gideon Moi kuwania kiti cha Seneti ya Baringo katika uchaguzi mdogo wa Novemba kulifanywa bila kuhusisha wanachama na uongozi wa chama.
“Hatuwezi kupuuza watu wengi wa Kaunti ya Baringo waliokuwa tayari kumuunga mkono katika kuwania kiti cha Seneti. Hatujui walikubaliana nini na Rais na tuna hofu kwamba muungano huu ulikuwa kwa maslahi yao binafsi bila kuzingatia wakazi,” aliongeza.
Viongozi hao sasa wanamtaka mwenyekiti wa chama kufichua yaliyomo kwenye makubaliano hayo.
