Hofu mabadiliko yakitarajiwa KFS
Na WINNIE ATIENO
WASIWASI umewakumba wasimamizi wa Shirika la Huduma za Feri (KFS) nchini, huku serikali ikipanga kufanya mageuzi katika shirika hilo, wiki tatu baada ya ajali kutokea katika kivuko cha Likoni.
Aidha serikali inataka kuhakikisha utendaji kazi bora katika shirika hilo, huku ukaguzi wa matumizi ya fedha pia ukitarajiwa wakati wowote bodi mpya itakapozinduliwa.
Hatua hizo madhubuti zinajiri siku nne baada ya bodi ya shirika hilo kubanduliwa na Rais Uhuru Kenyatta, kutokana na mkasa uliosababisha vifo vya mama na mwanawe, waliozama baharini katika kivuko hicho.
Ufichuzi huo umewaacha wasimamizi wa KFS katika njiapanda , kwa kuwa hawajui hatma yao, huku serikali ikiahidi kusafisha na kufanya mageuzi katika shirika hilo, ambalo linasimamia huduma za feri katika kivuko cha Likoni.
“Kama serikali tutahakikisha kuna mageuzi katika bodi mpya. Tutahakikisha tunapata bodi ambayo hatua ya kwanza itakayochukua ni kuajiri wataalam ambao watasimamia shirika hili jinsi inavyotarajiwa,” alisema Waziri wa Uchukuzi, Bw James Macharia katika mahojiano na Taifa Leo.
Alisema usimamizi unaotarajiwa kuteuliwa utapaswa kusimamia KFS kitaalamu.
KFS imekuwa ikimulikwa baada ya vifo vya abiria hao wawili waliokuwa wakivuka feri wakiwa kwenye gari lao la kibinafsi.
Mnamo Septemba 29, biwi la simanzi lilitanda nchini baada ya Mariam Kighenda na mwanawe Amanda Mutheu, walipozama baada ya gari lao kuteleza kutoka kwenye feri ya MV Harambee ikiwa katika kivuko cha Likoni na kutumbukia baharini.
Miili yao ilitolewa wiki mbili zilizopita na kuzikwa kwao kaunti ya Makueni mwishoni mwa juma lililopita huku Wakenya wakililia haki kwa wendazao.
KFS ililaumiwa kwa utepetevu na kushindwa kuopoa miili hiyo jambo lililolazimisha serikali kuingilia kati katika shughuli hiyo ambayo ilikuwa imezua hisia kali miongoni mwa Wakenya.
Ajali hiyo ilibaini ulegevu wa KFS kushindwa kushughulikia ajali au matukio ya dharura baada ya kuibuka shirika hilo halina kundi la waokoaji wala halilengi kuwa nao hivi karibuni, hata ingawaje ni wazi kuwa hali hiyo inahatarisha maisha ya maelfu ya abiria wanaotegemea kivuko hicho.
Kipindi cha miaka mitatu
Pia ilibainika kuwa feri zilizoharibika zilikuwa zinaendelea kusafirisha watu licha ya KFS kutumia Sh600 milioni kuzirekebisha katika kipindi cha miaka mitatu.
Ijumaa, Rais Kenyatta alibandua bodi ya KFS iliyokuwa ikiongozwa na mwenyekiti wake, Bw Dan Mwazo ambaye alikuwa amehudumu kwa miezi minne tangu ateuliwe na rais Juni mwaka huu.
Wengine walioathirika ni pamoja na Bi Daula Omar, Bi Naima Amir, Bi Rosina Mruttu na Bw Philip Ndolo.
“Bodi mpya inatarajiwa kufanya mageuzi bora katika shirika hilo ili kuhakikisha utendakazi bora na usalama wa abiria wetu. Kama wizara tumekubaliana kusaka bajeti kuimarisha KFS kama dharura,” alisema Bw Macharia.
Mwaka wa 2018, KFS ilipata faida ya Sh43 milioni tofauti na hasara ya Sh84 milioni mwaka wa 2017.
Bodi hiyo mpya pia itatwikwa jukumu la kupigia debe mradi wa vigari vya nyaya ambayo inatarajiwa kuimarisha uchukuzi katika kivukio hicho.
Feri ya MV Nyayo ina hitilafu.
Feri zingine ambazo zimekuwa zikihudumu licha ya kuwa na hitilafu za kimitambo ni pamoja na Mv Likoni na Mv Jambo.