Hofu ya usalama sensa ikianza
Na WAANDISHI WETU
NCHI nzima inapojitayarisha kwa shughuli ya kuwahesabu watu kuanzia leo Jumamosi jioni, hofu imeibuka kuhusu mikakati ya serikali ya kuwahakikishia Wakenya usalama.
Licha ya hakikisho la Waziri wa Usalama, Dkt Fred Matiang’i kwamba shughuli itaendeshwa chini ya ulinzi mkali, visa kadhaa vimeibua wasiwasi miongoni mwa wananchi katika maeneo tofauti nchini.
Tayari maafisa wa usalama wameeleza hofu kuwa huenda maeneo ya mipakani yakatumika kuwaingiza watu nchini kutoka nchi jirani kama vile Ethiopia na Somalia, ili kuongeza idadi ya watu katika baadhi ya sehemu.
Katika Kaunti ya Tana River, polisi wameonya kuhusu njama za kuigiza watu kutoka Somalia na Ethiopia ili kuhesabiwa.
Hii ni licha ya hakikisho kuwa Jeshi la Kenya (KDF) litadumisha usalama katika maeneo hayo.
Kwenye mahojiano na Taifa Leo, Kamanda wa Polisi wa Tana River, Bw Fredrick Ochieng’ alisema kuwa watu wanaingizwa nchini kutoka nchi hizo kupitia Kaunti-ndogo ya Bura na vijiji vilivyo karibu.
“Tuna ripoti za kijasusi kuwa baadhi ya watu wanaendesha njia za kichinichini za kuwaingiza raia wa kigeni nchini, hasa kutoka Ethiopia na Somalia ili kuongeza idadi ya watu katika wadi zao na maeneobunge,” akasema.
Alisema kwamba awali, polisi wanaolinda barabara ya Garissa-Madogo waliwakamata watu sita kutoka Ethiopia, walipokuwa wakielekea Tana River kutoka Mandera.
Alisema kuwa watu hao sita ambao ni wanaume ni wachache tu kati ya wengi ambao wamefanikiwa kuingia nchini bila stakabadhi zinazofaa.
Katika Kaunti ya Wajir, idara za usalama zimewekwa katika hali ya tahadhari baada ya mbunge wa Wajir Kaskazini, Ahmed Abdisalan na makarani wa kuhesabu watu kushambuliwa Alhamisi. Gari lake pia lilichomwa.
Alikuwa amefika katika eneo la Masalale kuwashinikiza wakazi kujitokeza ili kuhesabiwa. Gari la diwani mmoja pia liliharibiwa vibaya kwenye kisa hicho.
Kamishna wa Kaunti ya Wajir, Bw Loyford Kibaara alisema kwamba walinzi wake walifanikiwa kumuokoa.
Katika eneo la Kiamuri, lililo kati ya kaunti za Meru na Tharaka Nithi, wakazi walieleza hofu kwamba huenda Sensa ikakosa kusuluhisha mzozo wa mpaka ambao umekuwepo kwa muda mrefu.
Mchanganyiko wa jamii
Eneo hilo lina mchanganyiko wa jamii za Watharaka na Ameru, ambapo wote wanataka kuhesabiwa kuishi katika kaunti zao.
“Hatujui kitakachofanyika kwani wenyeji wa Tharaka wanataka kutambuliwa kuwa wanaishi katika kaunti hiyo, ilhali eneo hilo linachukuliwa kuwa katika Kaunti ya Meru,” alisema naibu wa chifu kutoka eneo hilo ambaye hakutaka kutajwa.
Licha ya hofu hiyo, Halmashauri ya Kitaifa ya Kukusanya Takwimu (KNBS) imewahakikishia Wakenya na wakazi wa Kaunti ya Nairobi kwamba shughuli hiyo itaendeshwa chini ya ulinzi mkali.
Mkurugenzi Mkuu wa halmashauri hiyo, Bw Zachary Mwangi alisema kuwa makarani wa kuuhesabu watu watavaa mavazi maalum na watabeba vitambulisho.
Vilevile, wataandamana na wazee wa vijiji, wasimamizi wa mfumo wa Nyumba Kumi, polisi na maafisa wa serikali.
Kulingana na taarifa za polisi, baadhi ya maeneo yanayohofiwa kutumika kuwaingiza watu hao ni Migingo, Msitu wa Boni, Mpeketoni na Isebania na mengineyo.