Homa ya China yazua hofu
ELIZABETH MERAB, NASIBO KABALE na SIMON CIURI
HOFU imezuka kuhusu uwezekano wa Homa ya China kusambaa nchini baada ya mwanafunzi aliyeshukiwa kuwa na dalili za virusi hatari vya Coronavirus kutengwa katika chumba maalum cha Hospitali Kuu ya Kenyatta (KNH) Jumanne.
Taharuki pia ilishuhudiwa katika Kaunti ya Kiambu wakati wafanyikazi wapatao 500 wanaojenga Bwawa la Karemenu walipohofia kuwa raia watatu kutoka China waliofika nchini Jumapili walikuwa wakiugua homa hiyo.
Kisa hicho cha mwanafunzi huyo wa kiume aliyetengwa KNH hakijathibitishwa lakini sampuli zilichukuliwa kwa uchunguzi wa kina.
Alikuwa amefika nchini Jumanne asubuhi kutoka China kwa ndege ya Shirika la Kenya Airways.
Hapo Jumanne wafanyikazi na wahudumu katika KNH walionekana kuchanganyikiwa na wenye wasiwasi baada ya mwanafunzi huyo kupelekwa huko moja kwa moja kutoka Uwanja wa Mdege wa Jomo Kenyatta (JKIA).
Shirika la ndege la Kenya Airways lilisema kuwa mwanafunzi huyo alitumia ndege yao KQ 886 kutoka mjini Guangzhou hadi Nairobi.
Walinzi katika chumba hicho cha wagonjwa wenye maradhi hatari ya kuambukiza, ambako mwanafunzi huyo ametengwa, walipewa vitambaa vya kujifunika mapua kama tahadhari wasije wakaambukizwa lakini wagonjwa na wahudumu wengine waliendelea na shughuli zao bila kinga.
Kisa hicho ni cha pili barani Afrika baada ya kingine pia cha mwanafunzi aliyekuwa akisomea China kuripotiwa Ivory Coast.
Maafisa wa matibabu Jumanne walikusanya sampuli kutoka kwa mwanafunzi huyo aliyetengwa KNH na kuzipeleka katika Kituo cha Kitaifa cha Homa kwa uchunguzi zaidi.
Mamilioni ya watu nchini China wamekatazwa kusafiri katika juhudi za kuzuia kusambaa kwa virusi hiyo.
Chama cha Madkatri (KMPDU) kilihimiza wahudumu wa afya wapewe vifaa vya kujikinga wasiambukizwe na pia kikawataka wachukue tahadhari wanapohudumia wagonjwa walio na dalili za homa.
Ugonjwa huo ulioripotiwa kwanza nchini China mnamo Desemba mwaka jana una dalili kama za nimonia, na umeenea hadi mataifa 16 kufikia jana, na ulikuwa umeripotiwa kuua watu 106 nchini China huku idadi ya walioambukizwa ikifika 4,500.
Maafisa wa afya nchini humo walisema wengi wa waliokufa ni wazee pamoja na watu ambao tayari wamekuwa na maradhi ya kupumua.
Ugonjwa huo ambao unashukiwa ulianza kutoka kwa nyama ya nyoka ama popo, umesababisha wasiwasi kote duniani kutokana na kuwa dawa yake bado haijagunduliwa.
Kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO), ugonjwa huo una dalili za kupungukiwa na nguvu mwilini, joto jingi, vidonda vya koo na kikohozi kikavu. Dalili hizi zinafanana na za maradhi mengine ya kupumua, hali ambayo imefanya iwe vigumu kuutambua.
Katika tukio la Kiambu, Katibu wa wizara ya afya wa kaunti hiyo, Mary Wambui alisema maafisa wa afya walitumwa eneo la Gatundu Kaskazini kunakojengwa Bwawa la Karemenu ambapo waliwatuliza wafanyikazi na wakazi kwa kuwahakikishia wageni hao hawakuwa wakiugua.
“Maafisa wetu walizuru bwawa hilo ambapo waliwaondolewa wakazi hofu kuhusu maradhi hayo. Hata hivyo tuko macho,” akasema Bi Wambui.