Huenda asilimia 75 ya kampuni zikafungwa Juni – CBK
NA FAUSTINE NGILA
HALI ya uchumi nchini inazidi kudorora kutokana na makali ya janga la Covid-19, huku serikali ikionya huenda Wakenya wengi zaidi wakapoteza ajira kufikia mwishoni mwa mwezi Juni.
Kulingana na Gavana wa Benki Kuu ya Kenya (CBK) Dkt Patrick Njoroge, huenda asilimia 75 ya kampuni ndogo na zile za wastani zikalazimika kufunga biashara kutokana na ukosefu wa fedha mwezi ujao.
Akihutubu hapo jana kuhusu athari ya virusi vya corona kwa uchumi, Dkt Njoroge alisema kampuni hizo zinafaa kulindwa dhidi ya hatari ya kuporomoka kwani zinachangia pakubwa kwa kuinua viwango vya ajira pamoja na utajiri wa nchi.
“Uchumi ulitarajiwa kupata pigo zaidi kati ya Aprili na Juni, kutokana na mikakati ya kuzuia kuenea kwa Covid-19 iliyoathiri vibaya sekta za uchukuzi, biashara na hoteli. Hivyo, kiwango cha kukua kwa utajiri wa nchi kinaweza kupungua hadi asilimia 2.4 kutoka 5.4 mwaka uliopita,” akasema.
Na wakati huo huo, hoteli ya kifahari ambayo imekuwa ikihudumu humu nchini kwa miaka 116, Fairmont Norfolk, ilifunga hoteli zake na kuwatimua wafanyakazi wote.
Meneja wa hoteli hizo humu nchini Bw Mehdi Morad, alisema uamuzi huo ulifikiwa kutokana na hali kwamba haijulikani ni lini virusi vya corona vitadhibitiwa na watu kuruhusiwa kuendelea na biashara zao.
“Hatuna budi kufunga biashara kwa sasa. Inasikitisha kuwa hoteli zetu za Fairmont The Norfolk, Fairmont Safari Club zimesitisha huduma kutokana na virusi hivi na mafuriko ya hivi majuzi katika hoteli ya Fairmont Mara Safari Club,” alisema.
Katika sekta ya fedha, benki ya Equity jana ilitangaza kuwa faida yake baada ya ushuru imepungua kwa asilimia 14 kutokana na utoaji wa mikopo ya Sh3 bilioni kwa Wakenya kuwasaidia kukabiliana na hali ngumu ya uchumi katika kipindi hiki cha Covid-19.
Hata hivyo, CBK imeweka asilimia 7 kama kiwango cha riba kwa benki za humu nchini, ili kuwezesha wawekezaji kuomba mikopo nafuu, na kuendelea kufanya biashara na kulipa wafanyakazi.
Hata hivyo, kabla ya virusi vya corona fika humu nchini, hali ya uchumi tayari ilikuwa mbaya, kwaani kampuni nyingi zilikuwa zishawafuta kazi wafanyakazi wake, baada ya kulemewa na biashara.
Baadhi ya kampuni hizo ni Tuskys, Mumias Sugar, Tullow Oil, East African Breweries, Sportpesa, Southern Sun Mayfair Hotel, New KCC, Sameer Africa, Mediamax na nyinginezo.