HabariMakala

Huenda huu ndio mwisho wa dunia?

February 19th, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na WAANDISHI WETU

UGONJWA wa coronavirus uliochipuka China mnamo Desemba 2019 umeibua mjadala huku baadhi ya vyombo vya habari vikiutaja kama uliotabiriwa kama ishara ya mwisho wa dunia.

Uvumi huo umechochewa na kitabu kilichoandikwa 2008 na Sylvia Browne kinachoeleza kuwa mnamo 2020 kutazuka maradhi ambayo yatakuwa na dalili kama za homa ya mapafu (numonia).

“Hapo 2020 kutazuka maradhi ambayo yanafanana na numonia na yatasambaa kote duniani. Viini vyake vitashambulia mapafu na itakuwa vigumu kuutibu. Ghafla ugonjwa huo utatoweka kabla ya kuzuka tena miaka kumi baadaye,” kinasema kitabu cha Brownie kinachofahamika kama End of Days: Predictions and Prophecies about the End of the World (Siku za Mwisho: Utabiri wa Mwisho wa Dunia).

Maradhi ya coronavirus yana dalili kama za numonia ambazo ni pamoja na joto jingi mwilini, kukohoa na kushindwa kupumua.

Tayari watu 1,800 walikuwa wamekufa nchini China kutokana na ugonjwa huo kufikia Jumanne, 72,000 wakiambukizwa.

Maradhi hayo yamesambaa Hong Kong, Macau, Ufilipino, Japan, Ufaransa na Taiwan.

Habari za kutabiriwa kwa maradhi hayo zilitiliwa mkazo na kitabu kilichoandikwa mnamo 1981 na Dean Koontz cha The Eyes of Darkness ambacho kimetaja maradhi yaliyozuka China katika mji wa Wuhan, mahala ambapo coronavirus ilizuka mnamo Desemba 2019.

Kulingana na kitabu hicho cha ubunifu, maradhi hayo yaliyopewa jina la Wuhan-400 yalitengenezwa na wanasayansi wa China katika maabara moja jijini Wuhan kwa lengo la kutumika kama silaha ya kibayolojia.

Baadhi ya vyombo vya habari ukiwemo mtandao wa Express.co.uk nchini Uingereza nao umepiga hatua moja zaidi na kutaja nzige ambao wamevamia Kenya, Somalia na Ethiopia kuwa sehemu ya ishara kuwa dunia inaelekea mwisho wake.

Hapo Jumanne, maafisa wa afya katika Kaunti ya Kitui walisema kuwa raia wa China aliyetengwa baada ya kutoka ziarani China na kurejea anapofanya kazi katika kampuni ya ujenzi ya Sino Hydro eneo la Mutomo ataendelea kutengwa kwa kwa wiki mbili.

Mwanamume huyo ambaye ni mhasibu katika kampuni hiyo inayojenga barabara ya Kitui-Mutomo-Kibwezi, alikuwa ameibua taharuki katika kambi anakofanyia kazi eneo la Mutomo, wakati wasimamizi wake kazini walipoagiza atengwe alipofika nchini Jumapili.

Afisa Mkuu wa Afya Kitui Richard Muthoka alisema Mchina huyo hakuwa na dalili za coronavirus, japo ataendelea kutengwa kwa wiki mbili ukamilike. “Amepimwa na madaktari wetu na kupatikana hana dalili za virusi vya corona,” Dkt Muthoka akasema.

Mwanamume huyo alisafiri kwa teksi hadi Mutomo kutoka JKIA, baada ya madereva wa kampuni yake kukataa kumbeba, kwa hofu ya kuambukizwa ugonjwa huo.

Wakati huo huo, idadi ya kaunti zilizovamiwa na nzige imefika 22 huku mashirika ya kimataifa yakionya kuhusu uwezekano wa wadudu hao kuongezeka kuanzia mwezi ujao msimu wa mvua utakapoanza.?

Jumanne, wakazi wa eneo la Muhoroni katika Kaunti ya Kisumu walisema nzige walianza kuingia eneo hilo wiki mbili zilizopita lakini jana idadi yao iliongezeka.

Wataalamu kutoka mashirika ya Chakula na Kilimo (FAO), Mpango wa Chakula Ulimwenguni (WFP), Ilani za Njaa (FEWS NET) na Mamlaka ya Ushirikiano wa Maendeleo Kiserikali (IGAD) zilisema kuna uwezekano mkubwa msimu wa mvua utakapoanza, nzige watataga mayai zaidi na kuendelea kuenea.

“Gharama ya kutoa misaada ya chakula itakuwa kubwa zaidi kuliko ile inahitajika kuangamiza wadudu hao. Kwa hivyo ni muhimu mataifa yajizatiti,” mashirika hayo yakasema katika taarifa ya pamoja.

FAO imeorodhesha Kenya, Ethiopia na Somalia kama mataifa ambayo yamo katika hatari zaidi Afrika Mashariki kukumbwa na kwa sababu ya nzige.

Ripoti ya FAO inaonyesha kaunti nyingine iliyoathirika majuzi zaidi ni Kericho ambapo wadudu hao walionekana Jumanne iliyopita.? Katika Kaunti ya Samburu, wadudu hao walivamia upya Kaunti Ndogo ya Samburu Mashariki wakitoka Isiolo.

Takwimu za Serikali ya Kaunti zilisema ekari zaidi ya 70,000 za mimea na lishe ya mifugo zimeharibiwa kufikia sasa katika kaunti hiyo.

Imefichuka kwamba baadhi ya wafugaji wameanza kuzozania lishe ya mifugo na kusababisha hofu ya ghasia.

“Jamii kutoka Samburu Mashariki tayari zimeanza kutoka eneo moja hadi jingine wakitafuta lishe na tunahofia hali hii inaweza kusababisha mapigano,” akasema Afisa Mkuu wa Mipango Maalumu katika kaunti hiyo Daniel Lesaigor.?

Kaunti nyingine zilizoathirika ni Kajiado, Makueni, Machakos, Embu, Kirinyaga, Kitui, Murang’a, Garissa, Meru, Isiolo, Mandera, Wajir, Turkana, Pokot Magharibi, Tharaka Nithi, Laikipia, Marsabit, Baringo na Tana River.