Huenda IEBC ikakosa kuunda maeneobunge, wadi za ziada kabla ya 2027
TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini (IEBC) huenda ikakosa kuunda maeneo bunge na wadi mpya kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2027 kutokana na hatua ya serikali ya kuchelewesha kuundwa kwa tume hiyo.
Spika wa Bunge la Kitaifa, Moses Wetang’ula alielezea hofu kuwa huenda tume hiyo ikakumbwa na changamoto si haba kwani bodi ya uchaguzi iliundwa kwa kuchelewa.
Uhakiki wa mipaka ya maeneobunge na wadi ulifanyika mara ya mwisho mnamo 2012, na kusababisha kuundwa kwa maeneobunge 290 kutoka 210.
“Hatua ya kuchelewesha kuundwa upya kwa IEBC kumekwamisha shughuli muhimu, ikiwa ni pamoja na mambo ya kuweka mipaka, ambao ni muhimu kwa mfumo wa uchaguzi nchini, pamoja na kuandaliwa kwa uchaguzi mdogo katika maeneobunge na wadi ambazo hazina viongozi,” akasema Bw Wetang’ula.
“Pia hatua hiyo huenda ikaathiri kuunda kwa maeneobunge ya ziada kabla ya uchaguzi mkuu wa 2027. Haiwezekani kwamba makamishna watapata muda wa kufanya mapitio ya mipaka kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2027. Tumepoteza muda mwingi kwa sababu ya kesi mahakamani. Hatujui kama kutakuwa na uwezekano wa kuundwa kwa maeneobunge ya ziada mara makamishna wapya watakapochukua madaraka,” akaongeza Spika Wetang’ula.
Hata hivyo, alisema kuwa marekebisho kulingana na idadi ya watu, yanaweza kuruhusu IEBC kuchora upya mipaka kwa kugawa upya idadi ya watu ndani ya maeneobunge yaliyopo.
“Mabadiliko ya pekee yanayowezekana yatahusisha marekebisho ya idadi ya watu, lakini itakuwa vigumu kuongeza jumla ya idadi ya maeneobunge,” akaeleza, akiwataka Wabunge kuunga mkono IEBC katika kutekeleza jukumu hilo mara makamishna wapya watakapoingia uongozini.
“Hatua hiyo itaathiri moja kwa moja uendeshaji wa uchaguzi na usahihi wa mipaka ya uchaguzi, ambayo ni muhimu kwa uwakilishi wa haki bungeni.”
Ibara ya 89 ya katiba kuhusu mipaka ya vitengo vya uchaguzi, inaeleza kuwa kutakuwa na maeneobunge 290 kwa madhumuni ya uchaguzi wa wabunge.