Huenda serikali iliuzia Wakenya kansa 2008
Na VALENTINE OBARA
HOFU imeibuka miongoni mwa Wakenya kwamba mahindi yenye sumu ya aflatoxin, yaliyoingizwa nchini kutoka ng’ambo miaka 10 iliyopita, ndiyo yamesababisha ongezeko la maradhi ya kansa nchini.
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Ubora wa Bidhaa Kenya (KEBS), marehemu Kioko Mang’eli alitabiri wakati huo kwamba kutakuwa na ongezeko la kansa nchini baada ya Wakenya kula mahindi hayo yaliyokuwa na sumu.
“Nina hakika kwa asilimia mia moja kwamba watu watapata magonjwa kati ya miaka 10 au 15 ijayo. Kutakuwa na maambukizi makali ya kansa kwa sababu wamekula mahindi yenye sumu. Watu wengi zaidi watakuwa hospitalini,” alitabiri Bw Mang’eli aliyefariki mapema mwaka huu.
Kashfa hiyo ilifanyika mwishoni mwa mwaka wa 2008 wakati serikali ilipoagiza magunia milioni tano ya mahindi kutoka Amerika na Afrika Kusini kukabiliana na uhaba mkubwa uliokuwa ukikumba nchi.
Huu ni mwaka wa 11 tangu Wakenya walipokula mahindi hayo, na tayari nchi imeshuhudia maambukizi ya juu ya kansa.
Usambazaji wa mahindi hayo yenye sumu ulikuwa mojawapo ya sakata kubwa zaidi za ufisadi chini ya utawala wa serikali ya mseto iliyoongozwa na Rais Mstaafu Mwai Kibaki na Bw Raila Odinga ambaye alikuwa Waziri Mkuu.
Bw Odinga na familia yake walikuwa miongoni mwa waliodaiwa kuhusika kwenye kashfa hiyo, pamoja na Naibu Rais William Ruto ambaye wakati huo alikuwa Waziri wa Kilimo, miongoni mwa wanasiasa na watumishi wengine wa umma.
Wote wamekuwa wakikanusha kuwa walihusika katika uagizaji huo kila wanapohojiwa kuhusu suala hilo.
Wabunge ambao baadhi yao walikuwa mawaziri, pamoja na maafisa wengine wakuu serikalini walihusishwa na utapeli katika uagizaji na uuzaji wa mahindi hayo yaliyoharibika.
Wakati Bw Mang’eli alipohojiwa na kamati ya bunge inayosimamia kilimo kuhusu sakata hiyo, alifichua KEBS haikuruhusiwa kukagua mahindi hayo.
Katika hali isiyoeleweka, mahindi hayo yalikaguliwa na Shirika la Kukagua Mimea la KEPHIS.
Kulingana na Bw Mang’eli, hii ilimaanisha mahindi hayo yaliruhusiwa kuingia sokoni bila hakikisho la ubora kwani KEPHIS ilikuwa na uwezo wa kukagua mimea na mbegu, wala si mazao ya nafaka ya kuliwa na binadamu.
Sumu ya aflatoxin hupatikana kwenye nafaka ambazo hazijakaushwa ipasavyo.
Kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO), athari zake kwa binadamu ni saratani, watoto kuzaliwa wakiwa na kasoro za maumbile, changamoto za kukua kwa watoto, na ukosefu wa kinga dhidi ya magonjwa mwilini.
Baada ya sakata hiyo kufichuka, Serikali ilichelewa kuagiza mahindi hayo yaharibiwe au kurudishwa katika nchi yalikotoka, na hivyo kiwango kikubwa kilisambazwa kwa wasagaji unga na kuliwa na Wakenya.
Wakati ukaguzi ulipofanywa katika bohari ya kampuni ya Grain Bulk Handlers, Mombasa baada ya kashfa hiyo kufichuka, ilipatikana hakukuwa na mahindi yaliyobaki humo.
Kwenye kashfa hiyo, badala ya Serikali kuuzia wasagaji unga mahindi hayo moja kwa moja, makampuni ya kibinafsi yaliyomilikiwa na wanasiasa na mabwanyenye wenye ushawishi, mengine hata yasiyohusika na masuala ya kilimo, ndiyo yaliyouziwa mahindi hayo.
Baada ya kununua mazao hayo yenye sumu kwa Sh1,700, makampuni hayo baadaye yaliwauzia wasagaji unga kwa kati ya Sh2,200 na Sh2,700.
Wiki iliyopita Mkurugenzi wa Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI), Bw George Kinoti alilaumu ulafi wa watu wachache kuwa chanzo cha ongezeko la kansa nchini.
Wachanganuzi wa kisiasa husema utapeli wa kuagiza bidhaa muhimu kutoka nchi za kigeni kiholela hutokea sana kabla au punde baada ya Uchaguzi Mkuu ili wanasiasa na wafadhili wao wapate fedha za kampeni ama kurudisha walizotumia.
Mwaka uliopita, hofu ilikumba taifa wakati serikali ilipofichua kiwango kikubwa cha sukari kilifika sokoni kikiwa na madini hatari kwa afya ya binadamu ya mercury.
Sukari hiyo iliingizwa nchini wakati serikali ilipofungua milango kwa wafanyabiashara mnamo 2017 kuagiza kilo 350 milioni za sukari kutoka nchi za kigeni bila ushuru kwa madai ilinuia kuepusha athari za ukame.