Habari

Huenda shughuli za kiuchumi zikafunguliwa kote nchini bila zuio na kafyu

May 23rd, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na MARY WANGARI

WAKENYA huenda wakarejelea maisha yao ya kawaida kipindi cha majuma machache yajayo pasipo kafyu na zuio la kuingia au kutoka katika baadhi ya kaunti, endapo kauli ya Rais Uhuru Kenyatta ni ya kuzingatiwa.

Akihutubia taifa kupitia taarifa iliyopeperushwa moja kwa moja kutoka Ikulu ya Nairobi mnamo Jumamosi, Mei 23, 2020, kiongozi wa taifa amesema wakati umewadia kwa taifa kurejelea maisha ya kawaida sawa na baadhi ya mataifa mengine duniani.

Rais ameeleza kwamba itakuwa muhimu Kenya kufungua tena shughuli zake za kiuchumi akifafanua kwamba taifa haliwezi kusalia katika hali ya kufungwa.

“Sisi kama serikali, kama serikali zingine za mataifa yote dunia nzima zimeanza kuona haja na hatuwezi kuendelea kusema Wakenya tukae nyumbani wala kuendelea kusema tu Wakenya msiende kufanya biashara, msiende kazini, namna hiyo,” amesema Rais Kenyatta.

Hata hivyo, ametahadharisha kwamba ili kufanikisha hatua hiyo, zitahitajika juhudi za kila Mkenya binafsi katika kuzingatia masharti yaliyotolewa na Wizara ya Afya.

Amewahimiza Wakenya kufuata masharti na kanuni za Wizara ya Afya ili kujikinga dhidi ya janga la virusi vya corona pamoja na kuwalinda Wakenya wenzao.

“Tukianza kupanua na kufungua uchumi wetu, wewe ujue ya kwamba, usipotii masharti yaliyopo sio wewe peke yako utaumia; unaumiza pia mwenzako kwa kazi ambayo unafanya. Ukienda nyumbani utaumiza mama na mtoto,” amesema.

Isitoshe, Rais amesema amejadiliana na maafisa wa afya na wadau wengine kwa lengo la kuhamasisha umma na kuandaa raia kurejelea maisha yao ya kawaida.

“Kwa hivyo, wakati umefika na nimeambia mawaziri na maafisa wetu wa afya waanze kuwaambia Wakenya kwamba hatuwezi kuendela na zuio – lockdown – na hatuezi kuendelea maisha na kafyu na tukifungua ni muhimu sote tuwe makini,” amesema.