Ibada ya Mazishi kuanzia Jumapili saa tatu chuoni JOOUST, Bondo
KAMATI ya Kitaifa ya Kuandaa Mazishi imetangaza kuwa ibada ya mazishi ya aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga itafanyika kuanzia saa tatu asubuhi Jumapili katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia ya Jaramogi Oginga Odinga (JOOUST), Bondo, Siaya.
Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari Oktoba 18, 2025 jioni, mwenyekiti mwenza wa kamati hiyo Naibu Rais Kithure Kindiki alisema kuwa ibada hiyo itaendelea hadi saa saba mchana.
“Baada ya hapo, kutafanyika shuhuda fupi, maombi na heshima za kijeshi kando mwa kaburi lake nyumbani kwa babake Kang’o Kajaramogi, kijiji cha Nyamira,” akaongeza.
Profesa Kithure aliongeza kuwa kamati hiyo anayoongoza pamoja na kakake Raila, Oburu Oginga, itatoa maelezo kuhusu shughuli zitakazofuata “kwa heshima ya marehemu Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga baada ya mazishi ya kesho”.
Awali, Katibu wa Usalama wa Ndani Raymond Omollo alitangaza mabadiliko mengine ya shughuli za kutoa heshima kwa mwendazake.
Kwa mfano, Dkt Omollo alitangaza kusikitishwa kwa shughuli ya kutoa nafasi kwa wananchi kutaza mwili wa Raila katika Uwanja wa Michezo wa Jomo Kenyatta, eneo la Mamboleo, Kisumu mwendo wa saa tisa alasiri.
“Mwili wa kiongozi wetu Raila Amollo Odinga utasafirishwa kwa helikopta hadi Bondo kutoa nafasi kwa wananchi wa eneo hilo kupata nafasi ya kuutazama,” akawaambia wanahabari katika uwanja huo.
Kulingana na mipango ya awali, wakazi wa Kisumu wangepata nafasi ya kuutazama mwili hadi saa tisa alasiri kisha usafirishwe kwa barabara hadi Bondo.
Shughuli ya kutazama mwili katika Opado Farm, Bondo ulikamilika dakika nne kabla ya saa moja za usiku, Jumamosi.