Habari

Idadi jumla ya visa vya Covid-19 nchini yagonga 781

May 15th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na SAMMY WAWERU

SERIKALI Ijumaa imethibitisha visa 23 vipya vya wagonjwa wa Covid-19 idadi jumla nchini Kenya ikifika 781.

Waziri msaidizi wa Afya Dkt Rashid Aman ametangaza akihutubia wanahabari katika makao makuu ya wizara jijini Nairobi.

Katika kipindi cha saa 24 zilizopita, sampuli 2,100 zimekaguliwa na kupimwa.

Kaunti ya Nairobi imekuwa na visa 11, Mombasa (5), Kajiado (3), Kiambu (2) na Wajir (2).

Watu watatu zaidi wamefariki kutokana na ugonjwa huu, idadi jumla ya waliofariki nchini ikigonga 45.

Maeneo ya mipakani yameendelea kumulikwa kutokana na ongezeko la maambukizi ya Covid-19 na sasa wizara imesema vituo tamba vya kupima virusi vya corona vitapelekwa katika eneo la mpaka wa Namanga ulioko baina ya Kenya na Tanzania ili kuimarisha mikakati iliyowekwa.

“Kuanzia juma lijalo tutapeleka vituo tamba katika kituo cha boda cha Namanga ili kuimarisha shughuli za kukagua na kupima madereva Covid-19,” amesema Dkt Aman.

Kituo hicho kinaendelea kumulikwa kutokana ongezeko la visa vya maambukizi ya virusi vya corona, miongoni mwa madereva wanaoingia humu nchini kutoka taifa jirani la Tanzania.

Serikali pia imesema inaendelea kuimarisha ulinzi katika maeneo ya mipaka ili kuzuia wanaoingia nchini kupitia njia za mkato.