Habari

IEBC haitakagua saini za BBI bila ya kupewa pesa

December 10th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) sasa inasema itaanza tu kukagua saini za kuunga mkono mchakato wa mageuzi ya katiba kupitia mpango wa maridhiano (BBI) baada ya kupokea ufadhili kutoka kwa serikali.

Mwenyekiti wa tume hiyo Wafula Chebukati jana alisema kuwa tume hiyo tayari imebuni kamati ya kusimamia shughuli hiyo itakayotoa nafasi ya kufanyika kwa kura ya maamuzi ya kuidhinisha mageuzi hayo.

“Kama tume kazi yetu inaaza sasa baada ya kupokea saini. Lakini kwanza, tutaomba fedha kutoka kwa Hazina ya Kitaifa. Tukipata fedha ndipo tataanza kazi ya kukagua saini hizo kwa sababu tayari tuko na kamati ya kura ya maamuzi ambayo itasimamia zoezi la ukaguzi wa saini hizo,” Bw Chebukati akawaelezea wanahabari.

Alisema hayo Alhamisi alipoongoza makamishna wenzake, Boya Molu na Abdi Guliye, kupokea saini 4.4 milioni kutoka wa wenyeviti wenza wa sekritariati ya BBI Denis Waweru na Junet Mohamed katika makao makuu ya tume hiyo Jumba la Anniversary, Nairobi.

Kaimu Afisa Mkuu Mtendaji wa IEBC Marjan Hussein Marjan pia aliwaongoza maafisa wa wengine kupokea sahihi hizo zilizokuwa kwenye masanduku 47 yenye majina ya kaunti zote nchini.

Hata hivyo, Bw Chebukati hakufichua kiasi cha fedha ambacho tume hiyo itaomba kufadhili zoezi la ukaguzi wa sahihi hizo akisema bajeti hiyo itakadiriwa na kamati ya maalum itakayosimamisha shughuli hiyo.

“Kamati hiyo itaketi leo na kesho (Ijumaa) kuandaa bajeti yake ambayo tutaandamanisha na ombi ambalo tutawasilisha kwa Hazina ya Kitaifa,” Mwenyekiti huyo akasema.

Bw Chebukati alifafanua kuwa wakati wa ukaguzi wa saini hizo, tume hiyo itahakikisha kuwa mswada ambao sekritariati ya BBI iliwasilisha ndiyo ile ambayo wapiga kura walizingatia walipokuwa wakitia saini zao.

Alipotakiwa kuthibitisha ikiwa kura ya maamuzi itagharimu Sh14 bilioni tume hiyo ilivyodai mwezi jana, Bw Chebukati alisema watatoa bajeti kamili ya shughuli hiyo baada ya mswada huo kuidhinishwa na angalau mabunge 24 ya kaunti na mabunge mawili ya kitaifa.

“Gharama kamili ya kura ya maamuzi itajulikana baada ya mswada wa marekebisho ya katiba kupitishwa katika mabunge huyo. Wakati huu siwezi nikatoa tathmini kamili ya fedha ambazo tutahitaji kuendesha shughuli hiyo,” akasema.

Mbw Waweru na Mohamed walisema kuwa waliwasilisha sahihi 4.4 milioni badala 5.2 zilizokusanywa baada ya “kuondoa zingine ambazo zilikuwa na dosari”.

“Leo Alhamisi tumewasilisha sahihi 4.4 milioni baada ya kufanya masahihisho machacha katika jumla ya sahihi 5.2 milioni tulizokusanya kutoka kwa Wakenya wanaounga mkono mageuzi ya Katiba ya BBI. Hata hivyo, ni sahihi 1 milioni pekee zinazohitajika kisheria kutuvukisha katika hatua nyingine,” akasema Bw Waweru ambaye zamani alikuwa Mbunge wa Dagorreti Kusini.

Wawili hao walielezea imani kwamba IEBC itaidhinisha saini hizo “haraka iwezekanavyo ili tuingia katika hatua nyingine.”

“Chebukati na wenzake watakuwa na kazi rahisi kwa sababu tumewasilisha pia nakala ya kidijitali kwa sababu tumekumbatia teknolojia ya habari katika shughuli zetu,” akasema Bw Mohamed ambaye ni kiranja wa wachache katika bunge la kitaifa na mbunge wa Suna Mashariki.

Bw Chebukati aliwaambia wanahabari kwamba IEBC itakuwa ikitoa habari za kila mara kuhusu mchakato wa ukaguzi wa saini hizo “ili kuzuia uwezekano wa Wakenya kupewa habari zisizo sahihi.”

Mwenyekiti huyo pia alisema mchakato huo utaendeshwa kwa kuzingatia masharti ya kuzuia msambao wa Covid-19.