IEBC yapuuza madai ya ODM kuihusu sajili
Na CHARLES WASONGA
TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imepuuzilia mbali malalamishi ya ODM kwamba haikutoa sajili sahihi ya wapigakura wa eneobunge la Kibra yenye maelezo yote inavyohitajika kisheria.
Kwenye taarifa aliyoituma kwa vyombo vya habari, mwenyekiti wa tume hiyo Wafula Chebukati amesema madai hayo ya ODM hayana ukweli wowote.
“Sajili kamilifu ya wapigakura ambayo tulitoa mnamo Oktoba 24, 2019, ina majina ya wapigakura, nambari zao za vitambulisho, nambari za vituo ambako watatekelezea haki yao ya kidemokrasia na nambari za usajili. Kwa hivyo, IEBC inapinga madai ya ODM kwamba ilitoa sajili ya wapigakura isiyo kamilifu,” akasema Bw Chebukati mnamo Ijumaa.
Hata hivyo, mwenyekiti huyo amesema kuwa kwa mujibu wa sehemu ya 34 (3) (4) ya sheria ya IEBC ya 2011 na kipengele cha 35 cha Katiba, tume hiyo iko huru kusitiri maelezo ya wapigakura ambayo huenda yakatumiwa kwa malengo mabaya.
“Hii ndiyo maana IEBC imetoa sajili ya wapigakura, lakini yenye nambari za vitambulisho vya kitaifa na nambari za simu zisizokamilika (truncated),” Bw Chebukati akaeleza.
Mwenyekiti huyo ameongeza kuwa mnamo Oktoba 30, 2019, IEBC iliweka nakala za sajili hiyo ya wapigakura katika vituo vyote vya kupigia kura katika eneobunge la Kibra ili wapigakura wapitie.
“Tulifanya hivyo, ili wapigakura waweze kupata fursa ya kuikagua na kuthibitisha kuwa maelezo yao yote ni sahihi. Na yeyote mwenye malalamishi yoyote anaweza kuyawasilisha katika ofisi yetu katika eneobunge la Kibra,” Bw Chebukati akasema.
Madai ya ODM
Mnamo Alhamisi ODM ilidai kuwa sajili ya wapigakura ambayo IEBC ilitoa haikuwa na maelezo yote.
Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari Katibu Mkuu wa chama hicho Edwin Sifuna alisema sajili kamilifu sharti iwe na “majina kamili ya wapigakura, kituo cha upigaji kura na nambari yake ya kitambulisho cha kitaifa.”
“Kile ambacho IEBC ilitoa mnamo Oktoba 24, 2019, ni sajili ambayo haina nambari za vitambulisho vya kitaifa; hali inayoifanya kuwa vigumu kwa wapigakura kuthibitisha maelezo yao. Kwa hivyo, shughuli nzima imegubikwa kwenye hadaa tupu,” akasema Bw Sifuna.
Chama hicho kiliipa IEBC makataa ya saa 24 itoe sajili sahihi la sivyo viongozi wake, kwa mara nyingine, waandamane hadi katika makao makuu ya tume hiyo jumba la Anniversary, Nairobi, “kuitisha sajili sahihi.”
ODM pia iliitaka IEBC kuelezea ni kwa nini majina ya wapigakura 19,200 yaliondolewa kutoka kwenye sajili.
Aidha, Bw Sifuna alidai kuwa majina ya watu 10,040 yalikuwa yameongezwa katika sajili hiyo huku watu 3,821 wakihamishwa kutoka vituo ambavyo wao hupigia kura hadi vingine, bila ufahamu wao.
Hata hivyo Ijumaa, Bw Chebukati amesema madai hayo ni “vitisho visivyo na msingi wowote.”
“Ukweli ni kwamba idadi kamili ya wapigakura katika eneo bunge la Kibra ni 118,658, kulingana na sajili iliyotumika katika uchaguzi mkuu wa 2017. Kufikia sasa wapigakura 333 zaidi wamejiandikisha, 50 wamehamishwa kutoka kituo kimoja hadi kingine na jina la mpigakura mmoja limefutwa,” akasema.
Bw Chebukati amesema kuwa tume haitakubali kutishwa inapotekeleza wajibu wake kulingana na sheria na Katiba ya nchi.
“Tumejitolea kutoa nafasi sawa kwa wagombeaji wote katika uchaguzi mdogo wa Kibra. Na tunatoa wito kwa wapigakura kujitokeza kwa wingi kuwapiga kura mnamo Novemba 7,” akasisitiza Bw Chebukati.