IPOA yachunguza OCPD Lang’ata kwa kuzuia haki Thompson Hull Limited
MAMLAKA Huru ya Kuchunguza Utendakazi wa Polisi (IPOA) imeanzisha uchunguzi (IPOA/CMU/003547/2025) dhidi ya madai kwamba Kamanda wa Polisi wa Kituo cha Lang’ata (OCPD) alijaribu kuzuia haki kutendeka kwa kuagiza kufukuzwa kwa kampuni ya Thompson Hull Limited kutoka katika mali inayozozaniwa mtaani Karen, Nairobi.
Uchunguzi huo unafuatia malalamishi yaliyowasilishwa na kampuni hiyo, ikidai kuwa OCPD alichukua hatua kinyume na uamuzi wa Mahakama ya Mazingira na Ardhi wa Septemba 26, 2024, uliokataa kuwarudisha Agnes Wachuka na Joseph Wambugu katika kipinde hicho cha ardhi cha nambari L.R No. 3589/47.
Katika barua kwa IPOA, ambayo Taifa Leo imeona, Thompson Hull Limited ilidai kwamba maafisa wa ngazi ya juu wa polisi waliagiza maafisa 15 kuwafukuza kwa nguvu wafanyakazi wake, kuwakamata walinzi wake, na baadaye kuwalazimisha kutoa taarifa za uongo.
Kampuni hiyo pia iliwashutumu maafisa hao kwa kuchukua pikipiki za walinzi wake na kutisha mashahidi, ikieleza vitendo hivyo kama jaribio la makusudi la kuzuia haki.
Kesi hiyo pia imeripotiwa kwa Kitengo cha Mambo ya Ndani cha Huduma ya Polisi ya Taifa kwa uchunguzi.
Kumbukumbu za mahakama zinaonyesha kwamba ombi la Wachuka na Wambugu kurejeshwa kwenye mali hiyo lilikataliwa ili kuepuka “mkanganyiko mkubwa zaidi” kabla ya kusikilizwa kwa kesi kamili.
Akijibu madai hayo, OCPD wa Lang’ata alikiri kupokea malalamishi hayo, lakini akakanusha kufanya kosa lolote. Alisema polisi huchukua hatua tu kwa misingi ya amri halali za mahakama. Alikaribisha uchunguzi huo, akibainisha kwamba “kufukuzwa ni suala zito sana” linalopaswa kufuata taratibu za kisheria.
Wakati huo huo, kesi tofauti iliyowasilishwa katika Kitengo cha Jinai cha Mahakama ya Milimani inaomba OCPD na OCS wa Kituo cha Polisi cha Karen waachilie pikipiki za Thompson Hull Limited zilizokamatwa Septemba 28, 2025, kwa hoja kwamba kuzuiliwa kwake kunaenda kinyume na haki za umiliki wa mali chini ya Kifungu cha 40 cha Katiba.