Ishara Naibu Rais anakwepa vikao vya Rais
Na CHARLES WASONGA
MASWALI yameibuka kuhusu sababu za Naibu Rais William Ruto kukosa kuhudhuria kikao cha Baraza la Kitaifa la Usalama (NSC) kilichofanyika Ijumaa katika Ikulu ya Nairobi baada ya kisa cha kwanza cha maambukizi ya virusi vya corona kugunduliwa nchini.
Miongoni mwa waliohudhuria mkutano huo, ulioongozwa na Rais Uhuru Kenyatta, ni pamoja na Mkuu wa Majeshi Samson Mwathethe, Inspekta Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai, Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kitaifa la Ujasusi (NIS) Wachira Kameru na Mkuu wa Utumishi wa Umma Joseph Kinyua.
Kulingana na kipengee cha 240 cha Katiba, Naibu Rais ni miongoni mwa wanachama wa baraza hili ambalo, kati ya majukumu yake ni hutathmini na kujadili masuala yanayoweza kuathiri usalama wa kitaifa.
Lakini mkutano wa NSC ulipokuwa ukiendelea, Dkt Ruto alikuwa ziarani katika kaunti ya Nandi ambako aliongoza shughuli mbalimbali, ikiwemo ile ya utoaji wa vyeti ya umiliki ardhi kwa wakazi mjini Kapsabet.
Vilevile, alitumia wakati huo kukaripia wabunge wa upinzani ambao wametishia kuwasilisha hoja ya kumng’oa mamlakani na maafisa fulani wa serikali aliodai wanahujumu ndoto zake za kuingia Ikulu 2022.
Ndiposa msomi Profesa Makau Mutua akashangaa ni kwa nini Dkt Ruto alikuwa akihutubia mkutano wa kisiasa mjini Kapsabet ilhali bosi wake, Rais Kenyatta, alikuwa akiongoza mkutano wa NSC katika Ikulu ya Nairobi kujadili kero ya homa ya corona.
“Inashangaza kwamba Naibu Rais William Ruto anahutubia mkutano wa kisiasa katika Kaunti ya Nandi akikashifu njama ya kuondolewa kwake afisini ilhali Rais anaongoza mkutano wa Baraza la Kitaifa la Usalama na wakuu wa usalama,” akaandika katika akaunti yake ya Twitter.
Kauli yake ilimkasirisha kiongozi wa wengi katika Seneti Kipchumba Murkomen aliyemtetea Naibu Rais, akidai huenda Dkt Ruto hakualikwa kikaoni.
“Rais ana uhuru wa kuamua wale ambao anataka waalikwe katika mikutano ya baraza la usalama,” Murkomen akamjibu Prof Mutua.
Hata hivyo, mchanganuzi wa masuala ya kisiasa na uongozi, Mark Bichachi, Jumamosi alipuuzilia mbali madai ya Bw Murkomen akisema, haja yake kuu ni kuendeleza dhana kwamba Dkt Ruto anaendelea kutengwa na Rais Kenyatta.
“Kimsingi, Naibu Rais hahitaji kualikwa katika mkutano wa baraza la kitaifa la usalama,” akasema.
Kauli ya Bw Bichachi inaungwa mkono na Bw Martin Andati aliyesema hivi: “Ni kinaya kwamba Dkt Ruto anakwepa majukumu yake ya kikatiba ilhali amekuwa akisisitiza kila mara yenye ndiye Naibu Rais aliyechaguliwa.”
Kando na mkutano wa NSC Alhamisi, Dkt Ruto pia alikwepa mkutano wa kamati maalum ya kupanga mikakati ya kupambana na kuenea kwa virusi vya corona, iliyoongozwa na Rais Kenyatta Jumatano.