Ishara viongozi wa Mlima Kenya wako motoni Gachagua akionyeshwa mlango
KIZAAZAA kilizuka katika kaunti ndogo ya Bahati mnamo Ijumaa Oktoba 11 kwenye hafla ya mazishi ya mama ya mbunge wa eneo hilo Irene Njoki baada ya umati kuzoma viongozi wanaoegemea upande wa Rais William Ruto kufuatia hatua ya wabunge kumuondoa afisini naibu wake Rigathi Gachagua.
Waombolezaji walielekeza hasira zao viongozi hao, kutokana na risala ya rambirambi ya rais iliyosomwa kwa niaba yake na Gavana wa Nakuru Susan Kihika.
Baadhi ya Wabunge waliohudhuria walilazimika kukatiza hotuba zao au kuachana na siasa umati ulipozomea kila aliyehutubu.
Gavana Susan Kihika alipopanda jukwaani, alikuwa na kibarua cha kuwashawishi wakazi kumruhusu kuwasilisha rambirambi za Rais Ruto.
Waombolezaji ambao hawakutaka kusikia chochote walimzomea na kumkejeli hali iliyomlazimu kuwasihi wamruhusu akamilishe ujumbe uliokusudiwa familia iliyofiwa.
Hali ya taharuki ilianza pale mbunge wa Ndia, Bw George Macharia Kariuki alipopongeza miradi ya barabara ambayo serikali inatekeleza kote nchini.
Viongozi wengine waliohudhuria mazishi hayo ni wabunge Oscar Sudi (Kapseret), Betty Maina (Murang’a), Ann wa Muratha (Kiambu), James Githua (Kabete) miongoni mwa wengine.