Itumbi kulala ndani Muthaiga akisubiri kufikishwa kortini
NA MARY WANGARI
ALIYEKUWA Mkuu wa Dijitali, Ubunifu na Mawasiliano ya Ughaibuni katika Afisi ya Rais Bw Dennis Itumbi anatarajiwa kufikishwa mahakamani Alhamisi baada ya kukamatwa Jumatano Julai 3, na maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) huku madai ya kumuua Naibu Rais William Ruto yakichukua mkondo mpya.
Bw Itumbi alitiwa mbaroni kuhusiana na uchunguzi unaoendelea wa barua yenye utata kuhusu njama za kumuua Naibu Rais William Ruto kwa mujibu wa ripoti. Alibambwa na maafisa wa kikosi cha Flying Squad jijini Nairobi ambao walimtosa ndani ya gari la serikali.
Ripoti zinaashiria kwamba alipelekwa katika Kituo cha Polisi cha Muthaiga ambapo anazuiliWa akisubiri kufikishwa kizimbani Alhamisi.
Haya yanajiri siku chache baada ya ripoti zilizochapishwa na gazeti la Daily Nation mnamo Jumapili Juni 30, kuashiria kwamba majasusi walikuwa wakiwafuatilia washukiwa wawili wakuu kuhusiana na barua hiyo inayotaja njama za kumuua Naibu wa Rais.
Japo taarifa hiyo ilidokeza kwamba washukiwa hao wawili ni wasaidizi wa Bw Ruto, haikufichua majina yao.
Kinaya ni kwamba, ripoti hizo zilifuatia na cheche za mashambulizi makali kutoka kwa Bw Itumbi kupitia mitandao ya kijamii huku akishutumu gazeti hilo dhidi ya kudunisha hadhi ya uanahabari.
“Walitaja mahali ambapo maafisa hao wanaodaiwa kusakwa wanafanya kazi. Tuko karibu kumi. Hakuna yeyote miongoni mwetu aliyepigiwa simu au kutumiwa ujumbe. Uanahabari wa kupakua na kubandika kutoka kwa duru zisizotajwa zinazodanganya haupaswi kupata nafasi,”
“Taaluma ya uanahabari inadhalilishwa zaidi wakati Daily Nation inaponakili habari na kuchapisha dai baada ya lingine lakini haijishughulishi ama kuwapigia simu au kuwatumia ujumbe maafisa katika afisi ya Rais wanaodai wanasakwa na maafisa wa DCI na wamo mafichoni…,” alifoka kupitia akaunti yake ya Twitter.
Mnamo Juni 24 mawaziri watatu walifikishwa katika makao makuu ya DCI kuhusu madai ya njama za kumuua Bw Ruto.
Ripoti kuhusu barua iliyodaiwa kuandikwa na waziri asiyejulikana kuhusu njama za kumuua naibu rais zilitikisa taifa zilipoibuka hivi majuzi..
Hata hivyo, ukweli wa barua hiyo ulizingirwa na utata baada ya wapelelezi kushindwa kupata nakala yake sawia.
Maafisa walikuwa wamedokeza kwamba walikuwa wametambua ilikokuwa imetoka barua hiyo tata na wahusika wangefikishwa mahakamani hivi karibuni.