Jaji alivyomnyima Raburu mamilioni ya Bazu
JAJI wa Mahakama Kuu, Linus Kassan, amefutilia mbali uamuzi wa mahakama ya hakimu ulioitaka kampuni ya mawasiliano ya Airtel Kenya kumlipa mtangazaji maarufu Willis Raburu Sh6.5 milioni kama fidia kwa madai ya kutumia alama ya biashara ‘Bazu’ bila idhini, akisema mahakama hiyo haikuwa na mamlaka ya kisheria kusikiliza kesi hiyo.
Katika uamuzi wake, Jaji Kassan alisema kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Alama za Biashara, masuala yanayohusu ukiukaji wa haki za alama ya biashara yanapaswa kusikilizwa na Mahakama Kuu pekee na si mahakama ya hakimu. Kwa hivyo, uamuzi uliotolewa na Hakimu Mkuu Mwandamizi Rawlings Musiega mnamo Machi 11, 2024, ni batili.
Kesi hiyo iliwasilishwa na Raburu mwaka 2023 katika Mahakama Kuu, lakini baadaye ilihamishiwa mahakama ya hakimu na jaji mwingine kwa madai kuwa mahakama ya chini ndiyo ilifaa kuishughulikia. Jaji Kassan alitaja uhamisho huo kuwa kosa lisilo halali kisheria.
Raburu alidai kuwa alama ya biashara ‘Bazu’ aliyosajili rasmi Aprili 13, 2021, ilitumiwa na Airtel kuendeleza kampeni ya intaneti kwa jina ‘Bazu bundles’ kuanzia Desemba 2022, bila idhini yake. Alisema hatua hiyo ilitoa taswira kwa umma kwamba alihusika au aliidhinisha huduma hizo, jambo lililomuathiri kibiashara.
Kwa upande wake, Airtel ilikana madai hayo ikisema neno ‘Bazu’ lilikuwa likitumika kwa miaka mingi miongoni mwa vijana nchini, hasa katika lugha ya sheng, likimaanisha mtu mwenye ushawishi, mkubwa au mwenye nguvu, hivyo haliwezi kumilikiwa na mtu mmoja. Kampuni hiyo pia ilisema kuwa alama hiyo ni ya matumizi ya kawaida na haiwezi kusajiliwa kibiashara.
Jaji Kassan alisisitiza kuwa hata kama Mahakama Kuu ndiyo ilihamisha kesi hiyo hadi mahakama ya chini, hilo halikumpa hakimu mamlaka ya kushughulikia kesi hiyo. Alisema kila mahakama hupata mamlaka yake kutoka kwa Katiba au sheria mahsusi, na si kwa kuelekezwa na mahakama nyingine.
“Itakuwa ni makosa kisheria kudhani kuwa maagizo ya mahakama ya juu yanaweza kuhalalisha mamlaka ambayo hayapo kikatiba au kisheria,” alisema Jaji Kassan.
Aidha, Airtel ilikataa uamuzi wa awali wa hakimu uliotambua Raburu kama mmiliki halali wa jina ‘Bazu’ na kusema kuwa alama hiyo ilitumika kwa muda mrefu na umma kabla ya Raburu kuisajili, hivyo haikuwa uvumbuzi wake wa kipekee.
Mahakama ya hakimu ilikuwa imekubali hoja za Raburu na kutoa fidia ya Sh6.5 milioni, ikisema kwamba Airtel ilijipatia faida kwa kutumia jina hilo kinyume cha sheria. Lakini uamuzi huo umebatilishwa.