Habari

Janga kuu mgomo ukianza

December 7th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

ANGELA OKETCH na STEVE OTIENO

HATARI kuu inakodolea macho taifa hili kuanzia leo Jumatatu endapo wahudumu wa afya watatimiza dhamira yao ya kuanza mgomo ili kuishinikiza serikali kuboresha mazingira yao ya kazi.

Madaktari, wauguzi, maafisa wa matibabu miongoni mwa wahudumu wengine katika hospitali za umma wamelalamika kuwa serikali imekataa kuwatimizia matakwa yao, ikiwemo kuwasambazia vifaa vya kutosha vya kujikinga wasiambukizwe na virusi vya corona wanapokuwa kazini.

Mgomo huo unajiri wakati ambapo maambukizi ya virusi vya corona yanaendelea kuongezeka katika kaunti kadhaa kama vile Nairobi na Mombasa, huku hospitali na vyumba vya kuwahudumia wagonjwa mahututi (ICU) vikifurika wagonjwa wa Covid-19.

Mgomo huo pia unajiri msimu wa sherehe za Krismasi na Mwaka Mpya ukianza, ambapo inatarajiwa viwango vya maambukizi vitaongezeka kwa sababu ya safari nyingi za watu na sherehe.

Kwa msingi huu, inatarajiwa kuwa mgomo wa matabibu utasababisha janga kubwa zaidi katika sekta ya afya ya umma ambayo tayari inatatizwa na vita dhidi ya Covid-19.

Kama ilivyo kawaida, watakaoteseka ni wananchi wa mapato ya chini ambao hawana uwezo wa kugharimia matibabu katika hospitali za kibinafsi.

Wahudumu wa afya wameathirika mno na janga hilo la corona kufuatia ongezeko la maambukizi na vifo miongoni mwao.

Wanachama wa vyama 16 vya kutetea maslahi ya wahudumu wa afya kote nchini wameapa kuanza mgomo wao kaunzia leo.

Mikutano kadhaa katika ya vyama hivyo na maafisa wa serikali kuu, kamati za bunge kuhusu afya, Hazina ya Kitaifa ya Bima ya Matibabu (NHIF), Baraza la Magavana na Tume ya Mishahara (SRC) haijazaa matunda yoyote.

Kaimu Katibu Mkuu wa Chama cha Madaktari Nchini (KMPDU) Chibanzi Mwachonda mnamo Jumamosi alishikilia kuwa mgomo utaendelea ikiwa wahudumu wa afya hawatapewa PPE, bima ya afya na marupurupu ya kufanya kazi katika mazingira hatari, miongoni mwa mahitaji mengine.

Vyama vingine vya wahudumu wa afya vinavyounga mkono mgomo huo ni pamoja na Chama cha Wahudumu wa Kimatibabu (KMA), Chama Kitaifa cha Wauguzi (KNUN), kile cha Maafisa wa Matibabu (KUCO) miongoni mwa vingine.

Wahudumu hao wa afya walisema PPEs zenye ubora wa chini wanazopewa wanapowahudumia wagonjwa wa corona ndizo zimechangia baadhi yao kupata maambukizi ya ugonjwa huo na kisha kufariki.

“Wanachama wetu wanahudumu katika mazingira magumu zaidi na hatari kwa muda mrefu,” akasema Dkt Mwachonda.

“Hatufutilia mbali mgomo hadi huo matakwa yetu yatimizwe. Matakwa hayo yanajumuisha uajiri wa madaktari 2,000 zaidi. Tulizipa asasi husika za serikali kuu na zile za kaunti muda wa wiki tatu kwa ajili ya mashauriano nasi lakini hazikutimiza matakwa yetu. Mgomo unaaanza usiku wa manane Jumapili,” akaongeza.

Dkt Mwachonda aliongeza kuwa wahudumu wa afya waliokodiwa kutoa huduma katika vituo vya karantini hawajalipwa wala hawana bima ya afya.

Katibu Mkuu wa KUCO, George Gibore alisema mgomo wao unaanza kesho Jumanne.

Aliambia Taifa Leo kwamba wanachama wake 37 wamelazwa katika hospitali mbalimbali nchini lakini NHIF imekataa kulipa bili zao.

Mnamo Jumanne wiki jana, Bunge la Kitaifa lilipitisha ripoti ya Kamati yake kuhusu Afya iliyopendekeza kuwa Hazina ya Kitaifa itoe Sh500 milioni za kufadhili bima ya afya kwa wahudumu wa afya miongoni mwa maamuzi mengine yenye manufaa kwa wahudumu wa afya.

Aidha, kamati hiyo inayoongozwa na Mwakilishi wa Kike wa Murang’a, Bi Sabina Chege iliamuru kwamba PPE zilizoko katika hifadhi za Mamalaka ya Dawa Nchini (KEMSA) na zilizonunuliwa kwa bei ghali zisambaziwe wahudumu wa afya.