Habari

Janga la bidhaa feki linavyoilemaza Kenya kiuchumi na kiafya

March 8th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na MWANGI MUIRURI

Kwa ufupi:

  • Nyingi ya bidhaa feki hasa vyakula, pombe na bidhaa za urembo hutengenezewa eneo la Kariobangi
  • Februari tahadhari ilitolewa kuhusu uuzaji wa kondomu feki, jambo ambalo linawaweka watumiaji kwenye hatari ya kuambukizwa maradhi ya zinaa
  • Sekta ya bidhaa feki imewatajirisha wahusika huku uchumi wa nchi na afya ya wananchi ikiwekwa kwenye hatari kubwa
  • Bidhaa feki zimeshuhudiwa katika dawa za magonjwa ya binadamu na mifugo, mbegu za mimea, mbolea, pombe, maji, vinywaji, vipuri vya magari na vifaa vya ujenzi 

WAKENYA wataendelea kukumbwa na ongezeko la maradhi yasiyo na tiba kama vile saratani, uhaba wa ajira, umaskini, ajali za barabarani miongoni mwa matatizo mengine iwapo biashara ya bidhaa feki haitakomeshwa.

Wadadisi wanaonya kuwa kabla ya 2030, sekta hii itakuwa kubwa kuliko ya bidhaa halali na hivyo kuwa na uwezo wa kulazimu maamuzi ya serikali mbali na kudhuru shughuli za kiuchumi na afya.

Kufikia sasa uuzaji wa bidhaa ghushi umekithiri katika nyanja nyingi hasa dawa za magonjwa ya binadamu na mifugo, mbegu za mimea, mbolea, pombe, maji, vinywaji, vipuri vya magari na vifaa vya ujenzi wa nyumba.

Hii inamaanisha kuwa Kenya itashuhudia ongezeko la magonjwa yasiyo na tiba kama vile saratani, uhaba wa chakula kutokana na mbegu na mbolea feki, vifo, kuporomoka zaidi kwa mijengo na ongezeko la ajali za barabarani.

Nyingi ya bidhaa feki hasa vyakula, pombe na bidhaa za urembo hutengenezewa eneo la Kariobangi. Ni vigumu kutofautisha bidhaa feki na halisi kwani upakiaji wake unaiga ule halisi.

Hii imefanya kampuni za bidhaa halali kubadilisha upakiaji kila mara katika juhudi za kukabiliana na bidhaa feki, suala ambalo linasababisha hasara kwao.

Madawa feki nayo huagizwa kutoka nje huku mengine yakitengenezewa nchini.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Afya, Sabina Chege anakiri kuwa kuna dawa feki zinazouzwa kwa wingi nchini, hali inayohatarisha afya ya umma.

Ni hapo Alhamisi tu ambapo Wizara ya Afya ilitangaza kuwa kuna dawa feki za kutibu sumu ya nyoka. Dawa hizo mbili zinafahamika kama Puff Under na Ant Venom.

Kondomu feki

Mwezi Februari kampuni ya PSI ilitoa tahadhari kuhusu uuzaji wa kondomu feki, jambo ambalo linawaweka watumiaji kwenye hatari ya kuambukizwa maradhi ya zinaa ukiwemo Ukimwi na mimba ambazo hazijapangwa.

Kwa mujibu wa Naibu Kamishna anayehusika na ukaguzi wa hesabu katika Mamlaka ya Ushuru Nchini (KRA), Bw Githii Mburu, uchumi unaathirika pakubwa kutokana na biashara ya bidhaa feki.

Anasema kuwa biashara hiyo inahusisha bidhaa ambazo hununuliwa kwa kasi sokoni hasa vileo, sigara na bidhaa za elektroniki akiongeza kuwa ni biashara yenye thamani ya mabilioni ya pesa.

Alisema kuwa kwa sasa KRA inachunguza kampuni zaidi ya 50 ambazo zinashukiwa kuhusika katika biashara hiyo haramu.

Mwenyekiti wa Kampuni ya utengenezaji vileo ya London Distillers, Mohan Galot anasema kuwa nusu ya vileo nchini ni feki na idadi hiyo inaendelea kuongezeka.

Mamilionea

Kulingana na Katibu Mkuu wa Muungano wa Watumiaji Bidhaa (Cofek), Stephen Mutoro, sekta ya bidhaa feki imewafanya wanaohusika kuwa mamilionea kwa haraka sana huku uchumi wa nchi na afya ya wananchi ikiwekwa kwenye hatari kubwa.

Aliyekuwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya kupambana na Mihadarati (Nacada), John Mututho anasema biashara ya bidhaa feki iko na uwezo wa kushinikiza ni nani anayechaguliwa katika vyeo mbali mbali na pia sheria na sera zinazowekwa.

Aliyekuwa Mbunge wa Kigumo, Bw Kihara Mwangi, ambaye ni mtaalamu wa ujenzi anasema visa vya mijengo kuporomoka vinatokana na utumizi wa bidhaa feki.

Mwenyekiti wa Muungano wa Matatu, Dickson Mbugua anasema ajali nyingi zina uhusiano na utumizi wa vipuri feki.