HabariMakalaSiasa

Je, ni nembo ya ‘usaliti’ kwa Raila kumkumbatia Uhuru?

March 18th, 2018 Kusoma ni dakika: 4

Na BENSON MATHEKA

Kwa ufupi:

  • Kuna hisia kuwa Bw Odinga ni mtu mbinafsi, asiyeweza kuaminika na lengo lake ni kuwatumia watu kuafikia malengo yake ya kisiasa na kisha kuwatema
  • Wanaodai Bw Odinga aliwasaliti vinara wenzake wanasema kwamba, matukio ya hivi punde ni historia inayojirudia katika maisha yake ya kisiasa
  • Mkutano wake na Bw Kenyatta umefananishwa na 2001 alipounganisha chama chake cha NDP na KANU ambapo aliingia serikalini kwa mara ya kwanza 
  • Peter Mathuki anasema japo Odinga amepigania demokrasia, uamuzi wake wa kujitenga na vinara wenza na kuzungumza na Rais Uhuru unamsawiri kama msaliti

HATUA ya kiongozi wa chama cha ODM, Raila Odinga, ya kujitenga na vinara wenza katika muungano wa NASA na kuamua kushirikiana na Rais Uhuru Kenyatta, imeibua tena nembo ya “msaliti” ambayo imekuwa ikimuandama katika vipindi tofauti vya maisha yake ya kisiasa.

Hisia za wanasiasa na wafuasi wa vyama vya Wiper, Amani National Congress (ANC) na Ford Kenya ni kuwa, Bw Odinga ni mwanasiasa mbinafsi, asiyeweza kuaminika na lengo lake ni kuwatumia watu wengine kuafikia malengo yake ya kisiasa na kisha kuwatema.

Kwa baadhi yao, Bw Odinga alichukua hatua hiyo ili kukwepa mkataba wa maelewano wa NASA, kwamba hatagombea urais 2022 na badala yake angeunga mmoja wa vinara wenzake.

“Usinitaje jina, lakini unaweza kuweka amana kauli hii; Bw Odinga anataka kukwepa mkataba wa NASA kwa sababu hakuwa, na hana nia ya kuunga vinara wenza 2022. Hivyo ndivyo alivyo na ndivyo amekuwa kwa miaka mingi,” anasema mbunge mmoja wa chama cha ANC na mshirika wa miaka mingi wa Bw Odinga.

Hata hivyo, wafuasi wa Bw Odinga wanaamini Bw Odinga ni mzalendo na kila hatua anayochukua ni kwa manufaa ya Wakenya. Wakereketwa wa chama cha ODM wanamtaja kama kiongozi jasiri asiyekosea katika kila hatua anayochukua na wameapa kumuunga mkono katika ushirikiano wake mpya na Rais Kenyatta.

“Nimesema mara nyingi kwamba, baba hawezi kukosea na nitarudia kusema hivyo.  Raila amejitolea mhanga kupigania demokrasia na haki za binadamu katika nchi hii na anajua afanyalo,” asema mwakilishi wa wanawake Kaunti ya Homa Bay, Gladys Wanga.

Hata hivyo, wanaodai Bw Odinga aliwasaliti vinara wenzake, Kalonzo Musyoka ( Wiper), Musalia Mudavadi ( ANC) na Moses Wetangula( Ford Kenya) wanasema kwamba, matukio ya hivi punde ni historia inayojirudia katika maisha yake ya kisiasa.

Wanasema hatua yake kumbukumbu ya alivyotofautiana na aliyekuwa makamu wa rais Michael Kijana Wamalwa 1994 muda mfupi baada ya kifo cha baba yake, Jaramogi Oginga Odinga aliyekuwa wakati huo kiongozi wa chama cha Ford Kenya.

Bw Wamalwa alirithi uongozi wa chama hicho kutoka kwa Jaramogi lakini kwenye uchaguzi wa viongozi, alimshinda Bw Odinga ambaye alihama na kujiunga na chama cha National Development Party (NDP).

 

1997

Kushindwa kwake na Bw Wamalwa kulimnyima tiketi ya kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu wa 1997. Katika NDP, alipata tiketi na kugombea urais lakini akawa wa tatu nyuma ya Rais Daniel Moi wa KANU na Mwai Kibaki wa chama Democratic Party.

Kutofautiana kwake na Bw Wamalwa ambaye alikuwa mwanasiasa muungwana kulimsawiri kama mwanasiasa mwenye tamaa ya uongozi ambaye hangekubali kuongozwa hata katika chama cha kisiasa na ndivyo ilivyo hadi wakati huu.

Mkutano wake na Bw Kenyatta umefananishwa na uamuzi aliochukua 2001 wa kuunganisha chama chake cha NDP na KANU ambapo aliingia serikalini kwa mara ya kwanza alipoteuliwa waziri wa Kawi.

Kulingana na wadadisi, japo lengo lake lilikuwa ni kupata tiketi ya kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2002 Moi alipokuwa akistaafu, yeye na wanasiasa wengine walipigwa kumbo Moi alipoamua kumuunga Uhuru Kenyatta.

Aliungana na wanasiasa wengine wa Kanu akiwemo Bw Musyoka, marehemu George Saitoti na Joseph Kamotho kupinga uamuzi wa Moi wa kuwataka wamuunge Bw Kenyatta ambaye walimchukulia kuwa limbukeni wa kisiasa wakati huo.

 

‘Kibaki Tosha’

Alivikwa nembo ya msaliti 2002 kwa kumtangaza Mwai Kibaki kuwa mgombea urais wa muungano wa upinzani  wa Narc siku chache kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka huo bila kushauriana na wanasiasa wenzake kwenye tamko maarufu la “Kibaki Tosha.”

Mdadisi wa siasa George Okwaro asema kwa kutamka Kibaki tosha, Odinga hakuwashauri wenzake na alionyesha kuwa mtu asiyetegemewa katika miungano ya kisiasa.

“Tamko hilo liliwakasirisha baadhi ya wanasiasa waliokuwa kwenye upinzani  na ukikumbuka baadhi yao, akiwemo Simeon Nyachae waliamua kujitenga na Narc na kugombea urais,” alisema Bw Okwaro.

“Kumbuka wakati huo, Bw Musyoka pia alikuwa na azima ya kugombea urais na kama wanasiasa wengine alihisi kusalitiwa,” aliongeza.

Kabla ya uchaguzi mkuu wa 2007, Raila alikuwa ametofautiana na Bw Kibaki na akaungana na wanasiasa wengine, akiwemo Bw Musyoka, Musalia Mudavadi na William Ruto kuunda chama cha ODM ambacho kilisajiliwa na watu wengine na wakalazimika kusajili ODM-K. Chama hicho kilikumbwa na misukosuko

 

Siasa si urembo

Bw Musyoka alitaka akabidhiwe tiketi ya urais ambayo Bw Odinga alimezea mate. Walitengana na Bw Odinga alipomweleza Bw Musyoka kwamba, siasa sio mashindano ya urembo mtu akabidhiwe tiketi kwa sababu ya kuwa na sura nzuri.

Kupitia juhudi na weledi wa siasa wa Bw Ruto, Raila alikomboa ODM alichotumia kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2007 uliokumbwa na utata naye Bw Musyoka akagombea kwa tiketi ya chama cha ODM- K ambacho alibadilisha kuwa Wiper Democratic Movement.

Kwenye  uchaguzi mkuu wa 2013, aliungana na Bw Musyoka na Bw Wetang’ula kuunda  muungano wa Coalition for Restoration of Democracy (CORD) na akateuliwa mgombea urais huku wakikubaliana kuwa angemuunga Bw Musyoka kwenye uchaguzi wa 2017. Hata hivyo, mambo yalibadilika Bw Mudavadi alipojiunga nao kubuni muungano wa NASA na Odinga akakabidhiwa tiketi kwa ahadi kuwa ingekuwa mara yake ya mwisho kugombea urais.

Kulingana na mkataba wa maelewano, kama NASA ingeshinda, Odinga angeongoza kwa kipindi kimoja na kumuunga Bw Musyoka au Bw Mudavadi. Hata hivyo, baada ya kushindwa na Rais Uhuru Kenyatta inaonekana alibadilisha nia na kuamua kwenda kinyume na matarajio ya wenzake.

Katibu mkuu wa chama cha Wiper Peter Mathuki anasema japo Odinga amepigania haki na demokrasia katika nchi hii, uamuzi wake wa kujitenga na vinara wenza na kuzungumza na Rais Uhuru unamsawiri kama msaliti.