Jeff Koinange taabani kwa kumuuliza Atwoli maswali ya chumbani
Na PETER MBURU
BARAZA la Uanahabari nchini (MCK) limetishia kumchukulia hatua kali mwanahabari Jeff Koinange pamoja na kituo cha runinga ya Citizen TV, kwa kukiuka maadili ya utendakazi.
Baraza hilo liliandikia mkurugenzi wa uhariri katika kampuni ya Royal Media Services (RMS) Joe Ageyo na Bw Koinange likitishia kuwaadhibu, kutokana na mahojiano aliyofanya mwanahabari huyo na kiongozi wa Muungano wa Wafanyakazi (COTU) Francis Atwoli.
Kwenye barua hiyo ya Agosti 16, 2018, afisa mkuu mtendaji wa MCK David Omwoyo anasema Bw Koinange alikiuka maadili ya uanahabari na sheria ya usiri wa kibinafsi.
Shirika hilo lilikerwa na Bw Koinange kumtaka Bw Atwoli kueleza ikiwa ni kweli amemwoa mtangazaji wa runinga ya KTN Bi Mary Kilobi, likisema Bw Koinange aliuliza maswali mengi ambayo ni ya kibinafsi, kama utofauti wa umri kati ya Bw Atwoli na Bi Kilobi.
“Lakini kazi bado unafanya? Katiba bado unasoma? Na kazi unaweza?” ni baadhi ya maswali ambayo mkuu huyo wa MCK alikerwa nayo.
Baraza hilo limemkosoa Bw Koinange kwa kuzungumzia masuala ya chumbani kwenye runinga, na katika wakati ambapo familia nyingi huwa zinatazama.
Wakati mmoja wa mahojiano hayo, Bw Atwoli alilazimika kumtahadharisha Bw Koinange kuwa maswali yake yalikuwa yamepotoka kwani kulikuwa na uwezekano kuwa pia wanawe (Atwoli) wangekuwa wakitazama mahojiano hayo.
Kwenye barua hiyo, Bw Omwoyo ameitaka RMS kumpokeza ripoti ya hatua ilizochukua ili kuhakikisha kuwa haitarudia makossa kama hayo siku za usoni.