Habari

Jeshi laua magaidi 4 waliovamia kambi yao

January 6th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

KALUME KAZUNGU na STEPHEN ODUOR

JESHI la Kenya (KDF) liliwaua washukiwa wanne wa al-Shabaab waliojaribu kuvamia kambi ya jeshi eneo la Manda, Kaunti ya Lamu Jumapili asubuhi.

Msemaji wa KDF, Kanali Paul Njuguna alisema kuwa wakati wa kutibuliwa kwa jaribio hilo la saa kumi na moja na nusu alfajiri, moto mkubwa ulizuka na kushika mapipa ya mafuta kwenye uwanja huo wa ndege, hivyo kusababisha moshi mkali.

Bw Njuguna alisema hakuna yeyote aliyejeruhiwa wala kuuawa kwa upande wa KDF waliokabiliana na kutibua uvamizi huo.

“Wanajeshi wetu walikabiliana nao na tayari miili minne ya magaidi imeonekana eneo hilo. Moto uliozuka ulikabiliwa na kuzimwa. Kwa sasa hali ni shwari na shughuli za kawaida zimerejelewa kwenye kiwanja hicho cha ndege,” akasema Bw Njuguna.

Hata hivyo, baadaye Halmashauri ya Kusimamia Safari za Ndege nchini (KCAA), ilitangaza kufungwa kwa uwanja huo.

Awali, duru za usalama zilisema kwamba magaidi wa Al-Shabaab walikuwa wamevamia kambi ya jeshi la Majini eneo la Manda-Magogoni na ile ya jeshi la Amerika, zote zikiwa kwenye kisiwa cha Manda-Bay, Kaunti ya Lamu.

Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Bw Irungu Macharia, alisema magaidi hao walivamia kambi hizo mbili majira ya saa kumi alfajiri na kufikia saa moja asubuhi, makabiliano bado yalikuwa yakiendelea.

Mwanamgambo wa kujitolea mhanga aliingia kambini na kujilipua na wengine wakajaribu kuingia kambini hapo kwa lazima. Wakazi wanaoishi karibu na kambi hizo pia walikiri kusikia milio ya risasi na milipuko ya mabomu kutoka eneo la kambi hizo.

“Tangu saa kumi na moja alfajiri, tumeamshwa na milio ya risasi na mabomu iliyotoka upande wa kambi ya jeshi. Pia tumekuwa tukiona wingu kubwa la moshi kutoka upande huo. Nashuku mambo si sawa eneo hilo. Huenda kuna uvamizi wa kigaidi. Tunawaombea wanajeshi wetu,” akasema Bw Paul Mwaniki.

Kutokana na tukio hilo, usalama uliimarishwa katika kaunti jirani ya Tana River na mpaka wa msitu wa Boni, baada ya wakazi wa Kilelengwani kuripoti kuwaona majeruhi wa al-Shabaab kijijini.

Kamanda wa polisi wa Tana River, Bw Fredrick Ochieng alisema ripoti ilipigwa katika kituo cha polisi cha Kilelengwani, ambapo mkazi mmoja alisema alikutana na washukiwa 11 akiwa anatafuta kuni msituni.

“Mkazi anasema jamaa hao walimkamata na kutisha kumuua iwapo atafichua habari kuhusu wao kuwepo kijijini,” akasema Bw Ochieng.