Habari

Jina la Waziri Mbadi latajwa kwenye kesi ya mauaji ya Sharon

Na RICHARD MUNGUTI May 22nd, 2025 Kusoma ni dakika: 3

MAHAKAMA kuu Jumatano (Mei 21, 2025), ilifahamishwa kwamba Waziri wa Fedha John Mbadi aliingilia kati kwenye mzozo wa urafiki kati ya aliyekuwa Gavana wa Migori Okoth Obado na marehemu Sharon Otieno kwa kuwateulia mpatanishi.

Aliyekuwa msaidizi wa Bw Obado, Michael Oyamo, alifichua hayo mbele ya Jaji Cecilia Githua akisema kwamba , Bw Mbadi alimteua diwani wa zamani marehemu Lawrence Mullah kuwapatanisha wapenzi hao.

Bw Oyamo anayeshtakiwa pamoja na Obado na mfanyakazi wa zamani wa kaunti ya Migori Casper Obiero alisema diwani huyo alikuwa atekeleze kazi ya kutafuta shamba kaunti ya Homa Bay na kumjengea Sharon nyumba.

Pia alikuwa anapewa pesa na Bw Obado kumpelekea Sharon za kujikimu kimaisha kwa vile alikuwa na ujauzito wake.

Msaidizi huyo wa Obado alieleza mahakama kwamba alipewa kitita cha kwanza cha Sh200,000 kumpelekea Bw Mullah amkabidhi Sharon aliyeuawa kinyama usiku wa Septemba 3 na 4 2018 katika msitu ulioko kaunti ya Homa Bay.

Bw Oyamo aliyeanza kujitetea Jumatano alisema alikutana na Bw Mullah, mwendazake Sharon na mwanahabari anayetambuliwa kwa herufi XYZ katika hoteli ijulikanayo kwa jina Tausi akiwa na ujumbe kutoka kwa Bw Obado.

Bw Oyamo alimkabidhi Bw Mullah kitita cha Sh200,000 naye akampa Sharon.

“Hizo pesa zilikuwa za kazi gani,” wakili anayemtetea Bw Oyamo alimwuliza.

“Pesa hizo nilizopewa na Bw Obado zilikuwa za kumpa Sharon ajikimu kimaisha kwa vile alikuwa mjamzito,” Bw Oyamo alijibu.

Aliongeza kusema Bw Oyamo alipewa kitita kingine cha Sh100,000 kumpelekea Sharon kupitia kwa Bw Mullah.

Aliwakuta XYZ , Mullah na Sharon na kumkabidhi pesa hizo.

Jaji Cecilia Githua anayesikiza kesi hiyo ya mauaji dhidi ya Obado, Oyamo na aliyekuwa mfanyakazi wa kaunti ya Migori Casper Obiero alielezwa “alimwandikia ujumbe wa shukran Bw Obado akisema alipokea kitita alichotumana.”

Baadaye, Oyamo aliambia mahakama mzozo ulizuka kati ya XYZ na Mullah kuhusu pesa hizo ambazo Obado alikuwa anamtumia Sharon.

Mahakama ilielezwa XYZ alikuwa hataki Mullah awe akipewa pesa hizo peke yake.

“Kwa nini XYZ alikuwa hataki Mullah apewe pesa hizo,” wakili anayemwakilisha Oyamo alimwuliza.

“Sharon alinieleza wawili hao walikuwa wanakosana kwa vile XYZ ndiye alikuwa achapishe katika Gazeti lenye ushawishi mkubwa urafiki kati yake na Bw Obado,” Bw Oyamo alisema.

Lakini akaongeza kwamba “Obado alikuwa amemwamuru awe akimpa Mullah pesa ampelekee Sharon.”

Msaidizi huyo alisema Sharon alimsihi Obado aitishe mkutano kati yake XYZ na Mullah kutatua mzozo kati ya wanaume hao wawili.

Aidha Sharon alimtaka Gavana awe akimtumia pesa moja kwa moja kwa njia ya MPesa ama awe akimpa Oyamo.

Mahakama ilielezwa Oyamo alipanga mkutano kati ya XYZ, Mullah na Sharon ufanyike Nairobi.

Mnamo Agosti 23, 2018 Oyamo alimpelekea XYZ Sh22,000 za nauli yao watatu-XYZ, Sharon na Mullah wasafiri hadi Nairobi kukutana na Obado aliyekuwa anahudhuria mkutano wa Magavana (CoG).

Watatu hao waliabiri gari hadi Nairobi kukutana na Obado.

“Je ulijuaaje urafiki wa Sharon na Obado ulikuwa umevurugika,” wakili anayemwakilisha Oyamo alimwuliza.

Akajibu: “Ilikuwa Julai 2018 nilipopokea simu kutoka kwa nambari tatu ambazo sikuwa najua wenyewe. Hatimaye walijitambua kuwa Sharon, XYZ na Mullah na kwamba walitaka kumwona Bw Obado, Gavana wa Migori wakati huo.”

Oyamo aliwataka wamfichuliwe sababu ya kutaka kumwona Obado.

Sharon alimweleza alikuwa na ujauzito wa Obado na alitaka amwone kwani alikuwa amemnyamazia.

Pia habari za mahaba kati ya Obado na Sharon zilikuwa zimesambaa katika mitandao ya kijamii na XYZ alikuwa anajiandaa kuichapisha katika chombo cha habari chenye ushawishi mkubwa.

Ni wakati huo alipokutana na XYZ, Sharon na Mullah kwenye hoteli ndipo akakubali kuwapeleka kwa gavana huyo wa zamani.

Jaji Githua alielezwa na Oyamo kwamba alimjulisha Obado habari hizo zilizokuwa zinasambaa ndipo akamfichulia Bw Mbadi alikuwa amemtuma mjumbe wake- Mullah- kuwapatanisha.

“Nimetatua suala hilo. Bw Mbadi amemtuma Bw Mullah kusuluhisha mzozo huo kati ya Sharon na Obado. Sharon alikuwa analalamika Obado amemnyamazia na alikuwa na mimba yake,” Oyamo alidokeza.

Shahidi huyo alisema aliendelea kufanya mkutano na Sharon na XYZ.

Watatu hao-Obado, Oyamo na Obiero wamekanusha walimuua Sharon na mtoto wake aliyekuwa na wiki 28 na kusalia muda mchache kuzaliwa.

Oyamo aliulizwa ikiwa anakumbuka kile viongozi wa mashtaka Gikui Gichuhi, Mercy Njoroge na Kigura Millicent walieleza korti kwamba “ushahidi walio nao umethibitisha yeye (oyamo) alihusika katika mipango ya kumuua kinyama Sharon.”

Alijibu kwamba anakumbuka viongozi wa mashtaka walisema watathibitisha kwamba yeye Oyamo aliwashawishi Sharon na XYZ wakutane na hatimaye akawakabidhi kwa wauaji.

“Niko mbele ya mahakama kujiondolea lawama na kuthibitisha mashahidi waliofika kortini walisema uwongo kunihusu. Ripoti ya DNA ilionyesha sikua na uhusu kimapenzi na Sharon. Mimba ilikuwa ya Obado,” Oyamo aliambia mahakama.

Kesi inaendelea kusikizwa leo Mei 22,2025.