HabariMakala

Jinamizi la pombe hatari Murang'a

July 20th, 2019 4 min read

Na MWANGI MUIRURI

KAUNTI ya Murang’a kwa muda sasa imekuwa ikekejeliwa kama iliyo na walevi ambao hutumiwa kujaribu makali ya kileo kipya sokoni.

Mwaka wa 2014 Kaunti ya Murang’a ilitangaza ulevi kuwa janga la kaunti.

Imekuwepo gumzo katika baadhi ya maeneo kote nchini kwamba walevi wa kutoka Murang’a wakionja pombe na waipitishe jua kwamba ina makali ya kukubalika na wateja wengine.

Wakiikataa, rejea kwa maabara yako uiimarishe.

Ni katika hali hiyo ambapo kwa sasa kuna msako mkubwa unaondelezwa baada ya kuripotiowa kuwa watu wawiwili wameaga dunia katika Kaunti ndogo ya Maragua baada ya kubugia pombe za sumu katika mtaa wa Gakoigo ulioko katika viunga vya mji wa Maragua.

Kwa mujibu wa Kamishna wa Kaunti hiyo, Mohammed Barre, wawili hao ambao ni wanaume wa kati ya umri wa miaka 28 na 32, waliaga dunia Jumanne na ambapo mara yao ya mwisho kuonekana walikuwa wameonekana wakibugia pombe za kipimo katika mtaa huo wa Gakoigo.

“Ripoti za kimatibabu zinaonyesha kuwa wawili hao walikuwa wamekanywa unywaji wa pombe kutokana na hali yao ya kiafya. Lakini walikuwa wakiendelea na kukaidi na ndipo walilemewa na athari za ulevi na wakaaga dunia,” akasema Barre.

Alisema misako iliyozinduliwa kutokana na tetesi zilizojiri za raia zimeishia kunaswa kwa washukiwa 106 tangu siku hiyo, wote wakiwa ni wale ambao wanakaidi masaa yaliyo halali ya kushirikisha biashara ya mabaa na pia walevi ambao wanakiuka sheria.

Ni hali ambayo imemshinikiza gavana Mwangi wa Iria kutoa ilani spesheli ya kuweka vikwazo vya kuzima biashara huru ya aina mbalimbali za pombe katika soko la kaunti hiyo.

Ilani hiyo inasema kuwa ni lazima baadhi ya wafanyabiashara wa kutengeneza pombe wawe wakisajiliwa na kutafuta idhini maalumu ya kuingiza bidhaa zao katika Kaunti ya Murang’a.

Ilani hiyo ambayo tayari imewasilishwa kwa kitengo cha utoaji leseni cha Kaunti hiyo inasema kuwa, “kila mfanyabiashara na kampuni yake ya pombe kwa pamoja wanafaa kutuma maombi rasmi kwa bunge la Kaunti hii kwa mujibu wa sheria mpya za pombe ambazo nimeidhinisha.”

Bunge la kaunti

Amesema kuwa bunge la kaunti ndilo litakuwa likitekeleza utafiti kuhusu ufaafu wa bidhaa hizo za pombe na hatimaye baada ya kuandaa mijadala bungeni, litakuwa na dhamana ya ama kupitisha au kuangusha maombi hayo.

Hatua hiyo amesema itawalenga wamilki wa viwanda vya kibinafsi vya kutengeneza pombe au mtu binafsi ambaye anajihusisha na uasambazaji wa pombe kwa kandarasi.

Amesema kuwa kampuni tajika ambazo zimetekelezewa ukaguzi wa ubora na ufaafu na serikali kuu hazitaathirika katika mwelekeo huu mpya wa masharti.

Yeyote atakayenaswa amekiuka sheria hizo atakuwa hatarini ya kutozwa faini ya Sh2milioni au kifungo cha miaka mitano gerezani.

“Wakati wamilki wa mabaa halali katika Kaunti hii wataamua kutusaidia kupambana na pombe hizo haramu, wateja watafurika katika mabaa yao hivyo basi kuzidisha faida zao. Kwa msingi huu, ni lazima pia wamiliki wa mabaa katika Kaunti hii wajumuishwe katika vita hivi,” akasema.

Alisema kuwa kwa sasa pombe haramu haswa zile zinazouzwa kwa chupa za plastiki huletwa kutoka Kaunti za Kiambu, Nairobi na Nakuru na akaonya kuwa serikali ya Kaunti hiyo itakuwa macho kuzima biashara hizo.

Mwakilishi wa wadi ya Ichagaki, Julius Ndung’u ambaye eneo lake limekuwa likiangaziwa mara kwa mara kama ngome ya biashara haramu ya pombe tayari ametangaza kuwa atakumbatia kwa dhati mwelekeo huo mpya wa Kaunti.

“Yeyote anayepambana na jinamizi la pombe haramu ni kipenzi kikuu kwa wadi yangu. Huyo ni wa kuungwa mkono hata ikiwa ni kwa vita vya kimwili. Atakayewaokoa vijana wetu kutokana na hatari ya pombe za mauti ni shujaa kwa macho yangu na ya wenyeji wa Kauntyi yote kwa ujumla,” akasema.

Sekta haramu ya pombe za sumu ikishirikishwa na ufisadi mkuu miongoni mwa maafisa wa kiusalama tayari imeorodheshwa kama iliyo na uwezo wa kumaliza watu 100, 000 katika Kaunti hii ya Murang’a kati ya 2019 na 2030.

Kwa mujibu wa aliyekuwa Mwenyekiti wa mamlaka ya uhamasisho na mapambano dhidi ya Ulevi (Nacada) John Mututho, kitaifa pombe hatari zinaua vijana 200, 000 kila mwaka, vijana ao hao wakifuja utajiri wa

Sh15 bilioni kila mwaka kusaka ulevi.

“Hizi ni takwimu ambazo nimeandaa kwa wizara ya masuala ya ndani nikiomba kuwe na mikakati maalum ya kupambana na kero hili. Ni takwimu ambazo tuliandaa kusaidia serikali kupambana na janga hili kati ya

2015 na 2020 lakini hakuna lolote limeonekana kutekelezwa,” akaambia Taifa Leo katika mahojiano maalum.

Bw Mututho alisema kuwa uchumi wa taifa kila mwaka hupoteza takriban

Sh10 bilioni zaidi katika sekta hii ya pombe za sumu.

“Hizo ni takwimu za kipindi hicho cha hadi 2020 ambapo tulidadisi kuwa uchumi hupoteza Sh5 bilioni kila mwaka kupitia bili za kiafya za waathiriwa wa pombe za sumu huku mauti yakiathiri familia hizo takriban Sh2 bilioni katika kipindi hicho nazo Sh3 bilioni zikipotea kutokana na ukwepaji wa kulipa ushuru kwa serikali kuu,” akasema.

Bw Mututho aliteta kuwa sekta hii ni vigumu kuithibiti kwa kuwa “imejaa mabwanyenye, maafisa wakuu serikalini na wakora wa kila aina ambao wako na uwezo wa kujikinga dhidi ya mkono wa sheria.”

Alisema kuwa Nacada nayo imetekwa nyara na mitandao ya ufisadi na haina uwezo wowote kwa sasa wa kutekeleza mikakati ya kuokoa taifa dhidi ya ulevi kiholela na unaosihia mauti, akiishutumu kwa kugeuka kuwa fisadi kwa hazina ambazo hupokezwa kupambana na janga hili la ulevi.

“Kwa sasa, wanaoendesha biashara hii ya mauti ni baadhi ya maafisa wa polisi, wengine ndani ya Nacada, walio katika mamlaka ya utoaji leseni katika serikali za Kaunti, baadhi ya wakubwa wa serikali za Kaunti na wafanyabiashara walio na pesa mfukoni kiasi cha kutowajibikia sheria,” akasema.

Bw Mututho alisema kuwa sekta hii ya pombe za sumu huwapa maafisa mafisadi takriban Sh100 milioni kwa siku kupitia hongo.

“Huu ni udadisi ambao ulifanywa na Nacada kwa ushirikiano wa Mpango wa kiusalama wa Nyumba Kumi mwaka wa 2018 ambapo maafisa wa usalama walikuwa wakipokezwa pesa tasilimu na mitandao ya pombe hizo za sumu ili kuilinda dhidi ya mkono wa sheria,” akasema.

Ni ufichuzi ambao aliyekuwa Mkurugenzi wa Nyumba Kumi, Joseph Kaguthi anaunga mkono akisema vita dhidi ya pombe za sumu, mara nyingi hulemazwa katika safu ya maafisa wa usalama.

“Jumbe kutoka mashinani kuhusu urejeo wa pombe hatari mwaka wote wa 2018 zilionyesha waziwazi kuwa maafisa wa usalama mashinani huzunguka kwa mabaa wakipokezwa hongo ili pombe hatari ziuzwe bila masharti,” akasema Kaguthi.

Anasema kuwa jumbe hizo zilikuwa zikiandamana na hata usajili rasmi wa magari ya polisi ambayo yalikuwa yakinaswa kila jioni yakizunguka mitaani kupokezwa mlungula wa kulinda hata walanguzi wa mihadarati, sio tu washirikishi wa pombe hatari..

“Hizi ni habari ambazo tulikuwa tunawapasha wakuu wa polisi ili wazishughulikie lakini hakuna la maana lilionekana kutekelezwa na kwa sasa, sekta ya pombe za sumu ni sawa na serikali mashinani,” asema Kaguthi.