Joho aagiza maafisa waruhusu wanachama na wafuasi wa 'Tangatanga' Mama Ngina Waterfront
Na MISHI GONGO
MKUTANO wa tatu wa hadhara wa uhamasisho wa ripoti ya mchakato wa maridhiano (BBI) unaandaliwa Mombasa, Pwani baada ya wa kwanza Kisii na wa pili uwanjani Bukhungu, Kakamega.
Gavana wa Kaunti ya Mombasa Hassan Joho ametoa amewataka maafisa wa usalama wahakikishe viongozi wanachama na hata wafuasi wa mrengo wa ‘Tangatanga’ unaomuunga mkono Naibu Rais William Ruto, wanaingia katika Mama Ngina Waterfront bila kusumbuliwa na kuzuiwa.
Aidha, wametakiwa wahakikishe viongozi wa Tangatanga wanaruhusiwa kuingia hadi jukwaani.
Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Seneti Kipchumba Murkomen, mbunge wa Malindi Aisha Jumwa, mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria, na mbunge wa Nyali Mohammed Ali ni baadhi ya wanaosawiriwa kuwa ni wafuasi wa Ruto ambao tayari wanahudhuria mkutano wa BBI Mombasa.
Aidha, matukio kadha ya mikasa yameshuhudiwa ambapo adhuhuri Taifa Leo imeshuhudia mwanamke akihudumiwa na maafisa wa Shirika la Msalaba Mwekundu baada ya kuzirai.
Vilevile walinzi wa viongozi wamelazimika kuondoa ngazi ya kupanda jukwaani ili kuzuia sehemu ya watu katika umati waliojaribu kufululiza hadi jukwaani.
Mlinzi wa mbunge wa Nyali ameondolewa kwa lazima jukwaani.