Joho ataka awamu ya pili ya SGR iahirishwe
Na WINNIE ATIENO
GAVANA wa Mombasa Hassan Joho amemtaka Rais Uhuru Kenyatta kusimamisha awamu ya pili ya mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kufuatia mikopo mikubwa ambayo serikali imechukua.
Gavana huyo alisema kukopa kwingi kutaathiri uchumi wa taifa sawia na maisha ya Wakenya endapo serikali itashindwa kulipa madeni hayo.
Akiongea baada ya kuwasili kutoka London, Uingereza, Bw Joho alisema serikali inafaa kutafuta njia mbadala kulipia madeni iliyochukua.
Awamu ya kwanza ya reli hiyo ya kisasa kutoka Mombasa hadi Nairobi iligharimu Sh327 bilioni, na kuipanua hadi Naivasha inagharimu Sh150 bilioni huku awamu ya mwisho ikikadiriwa kugharimu Sh380 bilioni.
Mwezi ujao, serikali inatarajiwa kutia saini kandarasi ya Sh380 bilioni kwa ujenzi wa awamu ya pili ya reli hiyo. Kwa jumla, mradi huo utagharimu Sh800 billion.
“Kama ni mzigo tusimamishe ujenzi wa SGR kwa muda waa miaka tano hivi. Tunafahamu Rais anataka kukumbukwa kwa mazuri baada ya kustaafu na ninamuunga mkono. Kwanini nijibizane na Rais anayeenda kustaafu?” akauliza Bw Joho.
Kwenye mahojiano na kituo kimoja cha Redio Mombasa, gavana huyo alisema ni sharti Rais atumie njia njema ya kuwacha hiba njema.
“Wacha urathi ambao hautawaumiza Wakenya. Tupunguze maswala ya kuzindua miradi badala yake tumalize miradi ambayo hatujamaliza. Tuwekeze fedha kwa mambo ambayo yatabadilisha hali ya maisha ya Wakenya,” akasema.
Bw Joho alisema anatamani kuchukua mkopo ili kuanzisha miradi kadhaa lakini hawezi sababu itawagharimu wakazi.
“Usiwape Wakenya mizigo mikubwa. Hii tabia ya omba omba imezidi sana katika serikali kuu, tujipange,” akaongeza.
“SGR ni mzigo kwa Wakenya na ikumbukwe kuwa mnamo 2016 tulitoa taarifa kuhusu SGR watu wakanicheka, niliposema huwezi kuchukua mkopo kutekeleza mradi kama wa SGR bila kuzingatia maswala mengine muhimu,” akasema Bw Joho.