Habari

Joto kuhusu ujenzi wa kanisa Ikulu

Na NDUBI MOTURI July 5th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

RAIS William Ruto ametetea ujenzi wa kanisa katika Ikulu ya Nairobi, akisisitiza kuwa anaugharamia binafsi na hakuna pesa za umma zinazotumika huku mradi huo ukizua mjadala mkali nchini.

“Mimi ni mcha Mungu na sina sababu ya kuomba msamaha. Tunajenga kanisa. Shetani akasirike afanye kile anachotaka kufanya,” alisema Ruto alipokutana na viongozi wa Embu katika Ikulu ya Nairobi.

Kiongozi wa taifa pia alisema aliamua kujenga kanisa hilo baada ya kubaini kuwa majengo mengi ya sasa katika Ikulu yalijengwa kwa mabati, hali ambayo haistahili hadhi ya Ikulu.

“Ninaambiwa hata kwenye magazeti kuna mtu anasema ninajenga kanisa hapa Ikulu. Ni kweli. Nilifika hapa Ikulu nikakuta kanisa lililojengwa kwa mabati. Hiyo kwa maoni yenu inafaa hadhi ya Ikulu? Situmii pesa za umma, natumia pesa zangu binafsi. Sijaanzisha kanisa jipya hapa, tatizo ni kuwa lilikuwa la mabati. Na Serikali ya Kenya haitalipia chochote,” aliongeza.

Hii inajiri huku baadhi ya viongozi, wataalamu wa sheria, na mashirika ya kijamii wakikosoa ujenzi huo, wakidai kuwa mradi huo unakiuka Katiba na kukuza ubaguzi wa kidini.

Wakili wa haki za binadamu Paul Muite alihoji mantiki ya kujenga jengo la kidini katika makao makuu ya utawala wa nchi.

“Hili kanisa ni la dhehebu gani? Wakatoliki hawataabudu katika kanisa ambalo halijabarikiwa. Waislamu wanahitaji msikiti. Wahindu wanahitaji hekalu. Ikulu ni ya Wakenya wote,” aliandika kwenye akaunti yake ya X.

Chama cha Wasioamini Mungu Kenya mnamo Ijumaa kilitangaza kuwa kitawasilisha kesi mahakamani kupinga ujenzi wa kanisa ndani ya Ikulu, kikiuitaja kuwa “kinyume na demokrasia” na hatua hatari kuelekea taifa la Kikristo.

“Ni jambo la kushangaza na lisilokubalika kuwa Rais William Ruto anajenga kanisa kwa siri katika Ikulu ya Nairobi,” alisema Harrison Mumia, rais wa chama hicho. “

Chama cha Democratic Action Party of Kenya (DAP-K) kinachoongozwa na Eugene Wamalwa pia kililaani mradi huo, kikimshutumu Rais kwa kupatia kipaumbele miradi isiyofaa wakati taifa linakabiliwa na matatizo makubwa ya kiuchumi.

“Wakati shule, hospitali na miundomsingi mingine muhimu inasambaratika, Rais anajenga kanisa la Sh1.2 bilioni katika Ikulu,” chama hicho kiliandika kwenye ukurasa wake wa X.

Kauli ya rais ilifuatia ripoti ya Taifa Leo kuhusu michoro ya kipekee ya usanifu wa jengo hilo, ikionyesha kuwa kanisa hilo ni sehemu ya mradi wa ukarabati unaogharimu mabilioni ya pesa katika Ikulu.

Jengo hilo, lililobuniwa na kampuni ya Skair Architects Limited, lina misalaba miwili juu ya paa lake na madirisha marefu na membamba yanayozunguka jengo kuu.

Mnara wa kati mrefu una msalaba mkubwa juu yake unaoashiria umuhimu wa kidini wa jengo hilo na kuonekana kutoka mbali.

Ndani ya kanisa hilo, kuna sehemu kuu ya ibada yenye uwezo wa kuketi watu 8,000, ikiwa na mistari minne ya viti. Pia, kuna milango mingi ya kuingilia, vyumba viwili vya maombi kila upande wa ukumbi mkuu wa ibada na vyumba vingine vya ziada vikiwemo ofisi na vyoo.

Gharama ya ujenzi wa jengo hilo inakadiriwa kuwa Sh1.2 bilioni, na linajengwa karibu na uwanja wa kutua helikopta wa Ikulu.

Mbunge wa Mumias Mashariki, Peter Salasya, alimuandikia Rais barua kali ya wazi.“Mheshimiwa Rais, Kenya ni taifa lisiloegemea dini yoyote. Kifungu cha 8 cha Katiba kinasema wazi: ‘Hakutakuwa na dini ya kitaifa.’ Wewe si kiongozi wa Wakristo pekee. Wewe pia ni rais wa Waislamu, Wahindu, wanaoamini mila, wasioamini Mungu, na kila imani nyingine nchini,” aliandika Salasya.

Wakili Ndegwa Njiru, alimlaumu Rais kwa kuwaibia Wakenya kupitia miradi mingi ya ujenzi, kutoka ukarabati wa Ikulu hadi ujenzi wa kanisa jipya. “Kenya inavuja damu, lakini umeamua kugeuza Ikulu kuwa eneo la ujenzi wa kudumu. Serikali yako ina vipaumbele visivyofaa kabisa! Kutoka ukarabati wa kila mara Ikulu hadi kujenga kanisa la Sh1.2 bilioni,” aliandika wakili huyo katika X.

Shule nyingi kote nchini zinakabiliwa na uhaba wa madarasa, vitabu, na walimu, huku hospitali za umma zikiendelea kukosa vifaa vya kisasa na dawa. Barabara na miundombinu mingine pia iko katika hali mbaya, jambo linaloathiri maisha ya kila siku na maendeleo ya kiuchumi.

Wakosoaji wanasema kuwa serikali inapaswa kuelekeza rasilimali zake kurekebisha miundombinu inayoporomoka na kuboresha huduma za umma, badala ya kufadhili mradi wa kifahari kama huu wa kanisa Ikulu.

Mnamo Juni 19, 2025, Bunge liliidhinisha Mswada wa Fedha wa kufadhili bajeti ya Sh4.29 trilioni.

Hata hivyo, hakuna ripoti rasmi zinazoonyesha kuwa Sh1.2 bilioni zilitengwa kwa ujenzi wa kanisa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026.

Licha ya kauli ya rais kwamba anatumia pesa zake binafsi, wakosoaji wa mradi huo wanasema iwapo hili litaruhusiwa kutokea, basi ina maana kuwa rais wa imani tofauti akichukua hatamu anaweza pia kujenga hekalu, msikiti au hata kanisa la dhehebu tofauti.

“Lakini, Ikulu si ardhi ya kawaida ya umma; ni ardhi ya umma iliyo chini ya ulinzi maalum kwa Rais pekee. Katiba iko wazi kabisa kwamba serikali lazima itenganishwe na dini.