Habari

JSC yadai mawasiliano na Jaji Koome yalinaswa na mtu asiyejulikana

Na JOSEPH WANGUI March 13th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

TUME ya Huduma za Mahakama (JSC) imeelezea wasiwasi kuwa njia zake rasmi za mawasiliano na Jaji Mkuu Martha Koome pamoja na majaji wa Mahakama ya Juu zimeingiliwa na mtu asiyejulikana, ambaye alidukua nyaraka muhimu.

Kupitia wakili wake, Issa Mansur, Tume hiyo Jumatano ilisema kuwa mvamizi huyo wa ajabu pia alipata taarifa za siri na nyeti zinazohusiana na mapendekezo ya kuwaondoa majaji saba wa Mahakama ya Juu afisini.

Hata hivyo, hakufichua aina ya taarifa za siri zilizodukuliwa, lakini alisisitiza kuwa kulikuwa na udukuzi wa mawasiliano rasmi pamoja na mfumo wa mtandao wa Idara ya Mahakama.

Haya yalifanyika kabla ya majaji wa Mahakama ya Juu kuwasilisha majibu yao kwa JSC kuhusu maombi matatu yanayolenga kuwaondoa afisini kwa tuhuma za utovu wa nidhamu, tabia mbaya na kutokuwa na uwezo wa kutekeleza majukumu yao.

Wakili Mansur alisema kuwa taarifa hizo za siri baadaye zilifikishwa kwa mkazi wa Narok, Bw Pariken Ole Esho, na kutumiwa kuandaa kesi ya kutetea majaji wa Mahakama ya Juu.

Kesi ya Bw Ole Esho imekitwa katika hoja kwamba JSC “haina taratibu za wazi na kanuni za kikatiba na utawala wa sheria kushughulikia malalamishi dhidi ya majaji, mahakimu na maafisa wengine wa mahakama.”

Mnamo Februari 18, Bw Ole Esho alipata maagizo kutoka kwa Mahakama ya Narok kuzuia majaji dhidi ya kufika mbele ya JSC katika kesi za kuwaondoa afisini zilizowasilishwa na Wakenya watatu wakiongozwa na aliyekuwa Waziri Raphael Tuju na mawakili Nelson Havi na Christopher Rosana.

Agizo hilo lilitolewa siku chache kabla ya tarehe ya mwisho iliyowekwa na JSC kwa majaji kuwasilisha majibu yao kwa malalamishi hayo.

Wakili Mansur alifichua haya mbele ya Jaji Charles Kariuki katika Mahakama Kuu ya Narok wakati wa kusikilizwa kwa kesi ya Bw Havi ya kuitaka kesi ya Bw Ole Esho itupiliwe mbali au ihamishiwe Nairobi ili iunganishwe na kesi nyingine saba kama hiyo.

Katika pingamizi dhidi ya kesi hiyo, Bw Havi aliambia korti Bw Ole Esho ni ajenti wa watu ambao hakuwataja majina.

Kwa mujibu wa wakili Mansur, Bw Ole Esho hajafafanua jinsi alivyopata taarifa za siri kutoka mawasiliano kati ya JSC, Jaji Mkuu na majaji wengine wa Mahakama ya Juu na kuzitumia kufungua kesi Narok.

“Kwa kukosa maelezo yanayoonyesha kuwa stakabadhi hizo zilipatikana kihalali, kesi hii inapaswa kutupwa. Watu hawawezi kudukua mtandao wa Mahakama ya Juu, kupata mawasiliano, na kuyatumia kuwasilisha kesi. Aliwezaje kudukua mawasiliano yaliyokuwa yameelekezwa kwa Jaji Mkuu, Naibu Jaji Mkuu, Ofisi ya Majaji wa Mahakama ya Juu na JSC? Kesi hii inapaswa kutupiliwa mbali na mlalamishi alipe gharama,” alieleza Bw Mansur.

Mawakili wa Bw Tuju walikubaliana na ombi la Bw Havi.

Wakili wa JSC pia alisema kuwa udukuzi huo ulifikia hadi kwenye mfumo wa mtandaoni ambapo mtu huyo asiyejulikana alipata stakabadhi zinazolindwa.

Alisema kuwa kuna mtu wa ndani mwenye ujuzi mkubwa aliyeweza kuingia kwenye Mfumo wa Ufuatiliaji wa Kesi za Mahakama (CTS).