Jubilee yamkana Khalwale
Na SHABAN MAKOKHA na CHARLES WASONGA
CHAMA cha Jubilee, kimekanusha kwamba kimemuidhinisha aliyekuwa Seneta wa Kakamega Boni Khalwale kuwa mgombeaji wa ugavana kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.
Siku moja baada ya Katibu Mkuu wa Jubilee Raphael Tuju kufichua kwamba chama hicho hakikuchangamkia Bw Khalwale, tawi la Kakamega limekataa kuwa mwanasiasa huyo atakuwa mwaniaji wa pekee wa tiketi ya ugavana katika kaunti hiyo.
Hii ni licha ya Dkt Khalwale kujiunga na Jubilee mnamo Mei 17 katika sherehe iliyoongozwa na Naibu Rais William Ruto katika eneo la Malinya.
Bw Tuju alisema hakuna mipango yoyote ya kumlaki rasmi mwanasiasa huyo katika makao makuu ya Jubilee, Nairobi kinavyofanyia wanasiasa wengine wenye ushawishi wakijiunga nacho.
“Dkt Khalwale hajapokewa rasmi katika chama cha Jubilee katika makao makuu yake eneo la Pangani, Nairobi. Na sina habari zozote kuhusu uwepo wa mipango kama hiyo,” Bw Tuju alisema alipoulizwa kama chama hicho kinapanga mapokezi rasmi ya Dkt Khalwale.
Ijumaa, mwenyekiti wa Jubilee tawi la Kakamega Bw Moses Lumiti pamoja na mshirikishi wa chama hicho eneo hilo Bw Raphael Werimo waliwaongoza wanachama wengine kupuuzilia mbali hatua ya Dkt Khalwale kujiunga na Jubilee na ndoto yake ya kutaka kuwania ugavana wa Kakamega 2022 kwa tiketi cha chama hicho.
“Jubilee ni chama kinachozingatia sheria na demokrasia. Tutafuata katiba ya chama kuwateua wawaniaji wa nyadhifa zote katika uchaguzi ujao,” alisema Bw Lumiti.
Bw Werimo alikanusha madai kuwa, Dkt Khalwale anapigiwa debe na Mbunge wa Mumias Mashariki, Bw Benjamin Washiali, ambaye ni kiranja wa wengi katika bunge la kitaifa.
“Hakuna kiongozi ambaye ana kibali cha kufanya maamuzi kwa niaba ya wengine,” akasema.
Maafisa hao waliwaomba wanachama wapya wanaojiunga na chama hicho kuzingatia sheria zake.
Dkt Khalwale alihama kutoka chama cha Ford-Kenya mnamo Mei 17 na kutangaza kumuunga mkono Naibu Rais William Ruto kuwania urais mnamo 2022 siku chache baada ya kuagizwa kujibu madai ya kukiuka wa kanuni zake.
Kauli ya Washiali
Akizungumza katika makazi ya Dkt Khalwale eneo la Malinya, Ikolomani, Bw Washiali alisema alikuwa tayari kuacha azma yake ya kuwania ugavana na kumuunga mkono.
“Jubilee inapaswa kuacha kufanya uteuzi wa mwaniaji wa ugavana katika Kaunti ya Kakamega na kumkabidhi tiketi Dkt Khalwale. Wale waliokusudia kuwania wadhifa huo pia wanapaswa kuacha ili kuepuka ushindani usiofaa,” alisema Bw Washiali.
Mbunge huyo alimtaja Dkt Khalwale kama mwanasiasa mwenye tajriba, baada ya kuwania wadhifa huo mnamo 2017.
Hata hivyo, Bw Werimo alisema Dkt Khalwale atazingatia kanuni za chama kama wanachama wengine.
Bw Raphael Tuju, amesema hakuna mipango maalum ya kumpokea rasmi Dkt Khalwale katika chama hicho. “Sifahamu kuhusu mipango yoyote ya kumpokea,” alisema kwenye mahojiano na Taifa Leo.
Katibu Mkuu wa Ford-Kenya Dkt Eseli Simiyu pia alisema kuwa chama hicho hakijapokea barua ya kujiuzulu ya Dkt Khalwale kama Naibu Kiongozi wake.