Habari

Jubilee yapangia Raila njama

July 13th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MWANGI MUIRURI

MRENGO wa Rais Uhuru Kenyatta katika chama cha Jubilee unapanga mikakati ya Kiongozi wa ODM Raila Odinga kuchaguliwa Rais 2022, lakini bila mamlaka.

Kundi hilo linaweka mipango kuhakikisha Mpango wa Maridhiano (BBI) unapitishwa ukiwa na kifungu cha kuleta cheo cha waziri mkuu mwenye mamlaka, ambapo wanalenga kuhakikisha wadhifa huo utapewa mtu kutoka Mlima Kenya.

Kwenye njama hiyo, wapangaji pia wanaangalia uwezekano wa Seneta wa Baringo Gideon Moi kuwa Rais, huku cheo cha Naibu Rais kikitengewa Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka.

Waziri wa Usalama Fred Matiang’i naye anatazamwa kama anayeweza kupokezwa cheo cha Naibu Waziri Mkuu.

Kulingana na aliyekuwa Mbunge wa Maragwa, Elias Mbau, tayari kuna mikakati maalum ambayo imewekwa ya kuandaa taifa kwa muungano wa kisiasa ambao utawaleta pamoja washirika wapya wa Rais Kenyatta na chama cha Jubilee ili waweze kuunga mkono mpangilio wa waziri mkuu kutoka Mlima Kenya.

Kati ya viongozi kutoka Mlima Kenya wanaoangaziwa kupewa cheo cha waziri mkuu ni aliyekuwa Mbunge wa Gatanga Peter Kenneth, Gavana wa Murang’a Mwangi wa Iria, Waziri wa Kilimo Peter Munya, Mbunge wa Kipipiri Amos Kimunya na Waziri wa Afya Mutahi Kagwe.

“Haya ni mambo ambayo yanapangwa na ndiyo sababu eneo la Mlima Kenya limekuwa likikumbwa na dhoruba kali la kisiasa huku baadhi ya wanasiasa wakijiweka tayari kupata baraka za Rais Kenyatta ili awasadie kukubalika na wakazi,” akasema Bw Mbau.

Alieleza Taifa Leo kuwa suala hili kwanza linahitaji BBI ipitishwe ndio kuundwe nafasi za kugawa mamlaka ya kitaifa kwa nia ya kuwaleta wengi iwezekanavyo pamoja.

“Serikali ikipanuliwa pale juu katika nyadhifa za kiutawala, utapata kwamba kila kona ya nchi itakuwa na uwezekano wa kuwa ndani ya serikali. Kukiwa na nyadhifa za Rais, Naibu wake, Waziri Mkuu na manaibu wake wawili, utapata kwamba Rais anajua afanyayo wakati unamwona akiwavuta wengi hadi ndani ya ushirika na Jubilee,” asema.

Naibu Mwenyekiti wa Jubilee, David Murathe anasema njama yao pia inalenga kuondoa dhana kuwa Wakenya wamechoshwa na uongozi wa watu wa Mlima Kenya.

“Ni wapi kuliandaliwa mkutano na Wakenya wakatoa maoni kuwa hawataki kuongozwa na mtu kutoka Mlima Kenya? Hakuna popote ndani ya sheria na kanuni za uchaguzi ambapo jamii za Mlima Kenya zimepigwa marufuku kuwania uongozi wa taifa hili,” akasema katika mahojiano na kituo cha redio cha Inooro.

Bw Murathe alisema kuwa sio lazima mamlaka ya kitaifa yatekelezwe na afisi ya rais ikiwa mtu kutoka Mlima Kenya hatakikani katika wadhifa huo, bali pia mamlaka hayo yanaweza yakatekelezewa katika cheo kingine mpya.

Mbunge Mwakilishi wa Wanawake wa Murang’a, Sabina Chege anatilia mkazo njama hii akisema Rais Kenyatta anajua afanyalo katika kuhakikisha anaacha serikali chini ya kiongozi anayetoka Mlima Kenya.

Kauli yake inaungwa mkono na Naibu Waziri wa Elimu, Zack Kinuthia aliyeambia Taifa Leo kuwa Rais Kenyatta yuko makini kuacha eneo Mlima Kenya katika “mikono dhabiti” kisiasa.

“Wale ambao kwa sasa wanalia kuhusu urithi wa 2022 hawajui mikakati inayopangwa. Lakini wakati itakapoanza kutangazwa kwa umma watapatwa na mshangao wa ajabu,” akasema Bw Kinuthia.