Juhudi za Ruto kumrudia Raila
Na JUSTUS OCHIENG
NAIBU Rais William Ruto anajaribu kurekebisha uhusiano wake na Kiongozi wa ODM, Raila Odinga ili kuimarisha nafasi yake ya kumrithi Rais Uhuru Kenyatta kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.
Duru zinasema kambi ya Dkt Ruto imekuwa ikifanya juhudi za kichinichini kurudisha uhusiano na upande wa ODM, ambao alishirikiana nao kwenye uchaguzi mkuu wa 2007.
Kati ya mambo ambayo yameonyesha Naibu Rais ameanza kulegeza msimamo kuhusu Bw Odinga ni tangazo kuwa anaunga mkono handisheki, kuandamana na Rais Uhuru Kenyatta na Bw Odinga majuzi kukagua ujenzi wa bandari ya Kisumu, kukoma kutumia maneno makali dhidi ya Bw Odinga pamoja na washirika wake wa kisiasa kusema wako tayari kufanya kazi na Bw Odinga.
Lakini upande wa ODM bado hauko tayari kumkumbatia Dkt Ruto kwa sababu wana shaka kuhusu iwapo kweli yeye na washirika wake wanamaanisha wanayosema.
Katibu Mkuu wa ODM, Edwin Sifuna alieleza Taifa Leo kuwa bado wana shaka kuhusu iwapo Naibu Rais kweli anamaanisha kuunga mkono handisheki, akisema watamwamini tu iwapo atatangaza hadharani kukomesha siasa za Tanga Tanga na kampeni za mapema za uchaguzi mkuu wa 2022.
“Sharti atangaze hadharani kuwa amekomesha kampeni za 2022 na kuwa yuko tayari kuunga mkono kufanikisha malengo ya handisheki na Ajenda Nne Kuu za Maendeleo,” akasema Bw Sifuna.
Naye Mwenyekiti wa ODM, John Mbadi alisema Dkt Ruto ameanza kutambua makosa yake ya kisiasa.
“Shida ya Naibu Rais ni kuwa aliharibu uhusiano wake na wanasiasa wakuu kama Raila na Uhuru, mfumo wa serikali na wananchi. Kwa wakati huu wananchi hawana haja na siasa za 2022,” akaeleza Bw Mbadi.
Alisema anashuku msimamo mpya wa Dkt Ruto akieleza kuwa huenda anafanya hivyo kufurahisha tu watu. Mbunge wa Kapseret, Oscar Sudi, ambaye ni mkereketwa wa Dkt Ruto, aliambia Taifa Leo kuwa kambi ya Naibu Rais iko tayari kufanya kazi na Bw Odinga kwa ajili ya chaguzi zijazo na maendeleo.
Naye mwenzake wa Soy, Caleb Kositany alisema: “Hatuna shida kufanya kazi na Bw Odinga. Siasa za Kenya hubadilika kila mara. Iwapo Uhuru anafanya kazi na Raila, nani basi hawezi akashirikiana na mwingine? Tuko tayari na tunaweza kushirikiana na yeyote akiwemo Raila.”
Msimamo wa sasa wa washirika wa Dkt Ruto ni tofauti na mbeleni ambapo walishikilia msimamo mkali dhidi ya Bw Odinga wakidai ana njama ya kuvunja serikali na kupata madaraka kwa njia za mkato.
Lakini Rais Kenyatta amekuwa akimtetea Bw Odinga akisema ushirikiano wao ni wa kuunganisha Wakenya na kufanikisha maendeleo.
Kulingana na mchanganuzi wa siasa, Bw Herman Manyora, hatua ya Dkt Ruto kulegeza msimamo imetokana na kutambua kuwa siasa zake kali zinavuruga ndoto yale ya kumrithi Rais Kenyatta.
Bw Manyora alisema hatua hiyo huenda ikawa ni mikakati ya kisiasa ama ameinua mikono.
“Labda ameona hataenda mbali akiendelea na msimamo wake mkali. Huenda amefahamu kwa kuendelea kupinga handisheki anajiharibia. Ama huenda alisema anaunga mkono handisheki kufurahisha watu,” akasema Bw Manyorta.
“Kupigana na mamlaka kuu sio jambo rahisi. Baada ya Gavana Waititu wa Kiambu kukamatwa alitambua Rais alimaanisha alichosema wakati alipotisha kuwachukulia hatua wanasiasa wa eneo la Kati wanaopiga siasa za kila mara,” akaongeza.