Habari

Jumwa apokewa kwa vifijo baada ya kutoka seli

October 18th, 2019 2 min read

Na MISHI GONGO

WABUNGE wa mrengo wa ‘Tangatanga’ walijiunga na Mbunge wa Malindi Aisha Jumwa, na kukashifu kukamatwa kwake wakidai kulifanywa kwa njia ya ubaguzi.

Wakiongozwa na Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Uasin Gishu, Bi Gladys Sholei, waliwalaumu polisi kwa kuwa na ubaguzi katika vita dhidi ya vurugu za uchaguzi.

Walitaka kujua ni kwa nini hakuna hatua iliyochukuliwa dhidi ya viongozi wa chama cha ODM, baada ya msafara wa McDonald Mariga anayewania kiti cha eneobunge la Kibra kwa tiketi ya Jubilee kupigwa mawe.

Hata hivyo, viongozi wa ODM Junet Mohamed, Babu Owino na Irshad Sumra, jana walihojiwa kuhusiana na maneno waliowaelekezea wabunge wa ‘Tangatanga’.

“Hivi karibuni wafuasi wote wa Naibu Rais wamekuwa wakinyanyaswa. Tunataka kuwahakikishia kuwa hatutatingika. Tutaendelea kumuunga mkono Bw Ruto hadi mwisho,” akasema Bi Sholei.

Wakati huo huo walimkashifu waziri wa Usalama, Dkt Fred Matiang’i wakidai anatumia mamlaka yake kudhalilisha wananchi wasio na hatia.

“Tumeregeshwa katika nyakati za Nyayo, ambapo watu waliteswa bila sababu wala maelezo,” akasema.

Hakimu Mkazi Mkuu, Bw Vincent Okello alitupilia mbali ombi la upande wa mashtaka kutaka mbunge huyo azuiliwe kwa siku 21 ili polisi wakamilishe uchunguzi.

Alisema polisi walipaswa kukusanya ushahidi wa kutosha wa kuweza kumshtaki kabla ya kumkamata mshukiwa.

“Polisi wanapaswa kuwa na ushahidi wa kutosha kabla ya kumfikisha mshukiwa mahakamani. Si kumleta kisha muanze kuomba mahakamani muda wa kuendelea kumzuia mshukiwa,” akasema.

Bw Okello aliwaamuru mbunge huyo na mlinzi wake Geoffrey Okuto wajiwasilishe kwa polisi wa upelelezi katika kesi hiyo Oktoba 22, ili kusaidia katika uchunguzi.

“Washukiwa watakuwa wanajiwasilisha mahakani kila wanapotakikana kwa uchunguzi wa kesi hii,” alieleza.

Bi Jumwa, alishtakiwa kwa madai kuwa alipanga kuvuruga uchaguzi mdogo wa Wadi ya Ganda, Kaunti ya Kilifi ambako mtu mmoja aliuawa Jumanne.

Mbunge huyo na mlinzi wake walikamatwa baada ya ghasia zilizotokea nyumbani kwa mwaniaji wa chama cha ODM kwenye uchaguzi huo mdogo, Bw Reuben Mwambize Katana.

Siku ya Jumatano, Mahakama iliagiza wazuiliwe hadi jana Alhamisi, ambapo ingetoa uamuzi wa iwapo ingekubaliana na polisi kuwazuilia kwa siku 21 au la.

Polisi waliambia mahakama kuwa wawili hao wanachunguzwa kwa mauaji ya Bw Gumbao Jola, mjombake mwaniaji wa ODM.

Kiongozi wa mashtaka Alloys Okemo, alisema wapelelezi wanamchunguza mbunge huyo kwa mauaji, kuchochea ghasia na kushambulia wananchi.

Alimtaja Bi Jumwa kuwa mchochezi na mpenda ghasia, akisema alivamia boma la Bw Katana akiwa katika msafara wa magari, akiandama na walinzi wake na kuwavuruga zaidi ya watu 500 waliokuwa mkutanoni.

Ripoti zinasema kuwa walipomuona mbunge huyo na walinzi wake, walianza kuwakemea na kuwarushia mawe na vifaa butu.