KAFYU: Wakenya watii amri, hali ya kawaida yarejea
NA FAUSTINE NGILA
Maisha ya kawaida yamerejea katika mitaa mingi mijini Jumamosi jioni, katika siku ya pili ya kafyu, baada ya Wakenya kutii amri ya kutotoka nje baada ya saa moja usiku.
Tofauti na Ijumaa jioni ambapo kulikuwa na purukushani katika maeneo mengi baada ya watu kushindwa kufika nyumbani kabla ya saa moja usiku, barabara zote na masoko yalibakia mahame Jumamosi usiku huku Wakenya wakisalia kwa nyumba zao.
Katika jiji la Nairobi, madereva walirejea kazini saa kumi na moja asubuhi Jumapili huku wengi wakitii sheria ya kutokaribiana.
Magari ya abiria 33, ingawa machache tu, sasa yalibeba abiria 16 Jumamosi jioni, kinyume na hapo Ijumaa ambapo yalizidisha idadi hadi abiria 40, hali iliyokiuka kanuni za kuzuia kuenea kwa gonjwa la corona.
Katika mji wa Mombasa shughuli za feri zilirejea saa kumi na moja unusu asubuhi na kufikia saa moja alfajiri kulikuwa na foleni ndefu katika kivuko cha Likoni waabiri wa feri wakisubiri kuvuka.
Unyama wa polisi uliojitokeza katika sehemu nyingi humu nchini kufuatia kafyu usiku wa Ijumaa uliyeyuka Jumamosi.
Video za polisi wakiwaadhibu vikali wakazi hapo Ijumaa hazikuonekana Jumamosi na huenda hali ikasalia hivyo katika siku zijazo.