Kafyu yaanza kwa machozi
SAMMY WAWERU, VALENTINE OBARA na MOHAMED AHMED
RAIS Uhuru Kenyatta mnamo Jumatano alitoa agizo la kutotoka nje kati ya machweo na macheo kama njia mojawapo ya kuzuia kuenea kwa Covid-19 nchini.
Katika Ikulu ya Rais jijini Nairobi, akihutubia taifa kwa njia ya mawimbi yaliyopeperushwa kupitia runinga, kiongozi wa nchi alitangaza kafyu ya kati ya saa moja jioni hadi saa kumi na moja asubuhi ambayo ilianza kutekelezwa Ijumaa, Machi 27, 2020.
Katika maeneo kama Mombasa, kulishuhudiwa vuta n’kvute baina ya raia na maafisa wa polisi muda wa saa chache kabla ya kuanza kwa kafyu ambapo watumiaji feri walihangaishwa; hasa katika kivuko cha Likoni.
Wakati wa kizaazaa hicho, mpigapicha wa kituo cha runinga cha NTV alihangaishwa na maafisa kumzuia kunasa picha za dhuluma zilizokuwa zinaendelezwa.
Agizo hilo la kafyu linaenda sambamba na sheria za Kenya, kifungu cha 57 cha Katiba ya sasa, ambapo Rais anaruhusiwa kutoa sheria ya aina hiyo ikiwa kuna janga linalotishia usalama wa taifa.
Kipengele cha 2 (g) – ulinzi wa usalama wa kitaifa, kinaeleza: “Sheria zitolewe ikiwa kuna hatari au janga la kitaifa, uharibifu wowote wa kitaifa unaojiri kupitia janga, likiwamo jangahai”.
Rais Kenyatta alitoa agizo la kafyu inayoendelea, baada ya kushauriana na Baraza la Kitaifa la Usalama (NSC), ambalo analiongoza kama mwenyekiti na Amiri Jeshi Mkuu, na linalojumuisha Naibu wa Rais, Dkt William Ruto, Wizara ya Usalama wa Ndani chini ya Dkt Fred Matiang’i, Katibu wake Dkt Karanja Kibicho, Inspekta Mkuu wa Polisi, IG, Hillary Mutyambai, miongoni mwa vigogo wa asasi kuu za usalama nchini.
Ni kafyu ya kitaifa nchini Kenya inayoibua kumbukumbu za ile ya mwaka 1982 wakati kulitokea jaribio la kuipindua serikali ya aliyekuwa Rais wakati huo Daniel Toroitich Arap Moi aliyefariki Februari 2020.
Hata hivyo, katika Kaunti ya Mandera na hata Lamu kumewahi kuwa na kafyu katika maeneo hayo hasa kama mkakati wa kukabiliana na
Rais mstaafu na ambaye kwa sasa ni marehemu, Daniel Toroitich Arap Moi alitoa amri ya kutotoka nje Agosti 1982, machweo hadi macheo, kufuatia jaribio la kutaka kumuondoa mamlakani pamoja na serikali yake. Ni kafyu iliyohusisha maafisa wa kijeshi, walioshika doria.
Ikizingatiwa kuwa baadhi ya Wakenya, hasa vijana hawakuwa wamezaliwa wakati huo, walio chini ya umri wa miaka 38, kafyu inayoendelea, wengi hawakuelewa amri ya aina hiyo inavyotekelezwa.
Dakika chache kabla ya saa moja za jioni, watu kadhaa walionekana wakiwa katika harakati za kuelekea nyumbani. Kwa waliodhani amri ya Rais ni ‘utani tu’, walijipata kuandamwa na maafisa wa usalama.
Maeneo ya miji, hususan jijini Nairobi wanaohitimisha gange zao usiku, hawakuepuka ‘makali’ ya polisi, picha na video za maafisa hao wakitandika raia kinyama zikisambaa mitandaoni. Aidha, baadhi ya matatu ziliagizwa kushusha abiria, wengi wakishangaa watavyofika makwao ilhali hawatakiwi kuwa nje.
Msemaji wa Polisi Charles Owino na ambaye aliungana na maafisa walioshika doria jijini Nairobi, alisisitiza sharti watu waheshimu sheria kwa kuwa hii ni operesheni kuokoa maisha na utani usiingizwe.
“Seli ni nyingi, tutakamata watu tuwafungie humo wafunguliwe mashtaka. Covid-19 si janga la kufanyia mzaha,” akaonya Bw Owino.
Licha ya mashirika ya kutetea haki za kibinadamu pamoja na wanasiasa kulalamikia oparesheni ilivyoendeshwa, Owino alisema maafisa wa usalama hawatalegeza kamba kutekeleza amri ya Rais akihoji wananchi wanachukulia virusi hatari vya Corona kama mzaha tu.
Kufikia mwendo wa saa tatu na nusu usiku, mitaa mingi Nairobi ilisalia kimya, wenyeji waliohesabika wakionekana kurejea. Ni kafyu iliyojiri kwa kishindo, mtaa wa Zimmerman, Githurai na Kasarani, sauti za mbwa zikihanikiza hewani kwa kile kilionekana kama kushangazwa na ukosefu wa watu kuwa nje.
Ni magari machache mno yaliyoonekana Thika SuperHighway, barabara ambayo kila sekunde na dakika, magari hupita kwa kasi.
Maeneo ya Tana River na Mlima Elgon – Bungoma, si mageni kwa kafyu, kufuatia kudorora kwa kiwango cha usalama.
Kafyu ya kitaifa inayoendelea nchini haijulikani itachukua muda upi, kufikia sasa Kenya ikithibitisha visa 31 vya Covid-19.
Mgonjwa mmoja wa Covid-19 alitangazwa kufariki mnamo Jumatano, Waziri wa Afya Mutahi Kagwe akieleza kwamba pia aliugua ugonjwa wa Kisukari.
Kati ya 31 hao, mmoja ametangazwa kupona, ingawa Waziri Kagwe amesema ataendelea kusalia hospitalini kufanyiwa vipimo kadhaa kuthibitisha ni salama.